Header Ads Widget

TANZANIA KINARA AFRIKA UJENZI WA MIUNDOBINU SEKTA YA AFYA



Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leornad Subi akizungumza na baadhi ya wahudumu wa afya mjini Kahama.
 Na Mwandishi Wetu-Shinyanga
Tanzania kwa sasa ni moja ya nchi bora Barani Afrika ambayo imewekeza katika miundombinu ya Sekta ya Afya kwa kiwango kikubwa ikiwa ni moja ya mafanikio makubwa kwa serikali ya wamu ya tano kwa sasa.

Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leornad Subi amesema hayo jana alipofika Wilayani Kahama kufanya ukaguzi shirikishi na kujionea miundombinu mpya ya Sekta ya Afya Wilayani Kahama.

Dkt. Subi alitaja lengo la Wizara ya Afya kufanya ukaguzi katika miundombinu ya Afya ni kuona huduma zinazotolewa katika sekta ya Afya inakizi viwango kwa lengo la kutoa huduma bora na za uhakika kwa wananchi.

Aidha Dkt. Subi aliongeza kuwa lengo kubwa la serikali ni kuona kuna ufanisi mkubwa wa huduma zianzotolewa katika miundombinu hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza vifaa tiba vitakavyowawezesha wahudumu wa Afya kutoa huduma zenye ubora ili kuhimarisha Afya za wananchi ikiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Dkt. Subi ameongeza kuwa ukaguzi wake katika hospitali ya Mji Kahama amegundua kuwa kuna mapungufu ya kiutendaji ambayo ni kutoweka vizuri kumbukumbu katika vitabu vya Mtua kwakuwa kuna masuala ya msingi ambayo wahudumu wa Afya wameonekana kutoweka kumbukumbu zake kama inavyotakiwa.

Pamoja na kubaini mapungufu hayo Dkt. Subi amelekeza wataalam wa Afya kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa madawa mara kwa mara na kuwasilisha taarifa ya ukaguzi huo kwa Mkurugenzi ili kuweza kukabiliana kwa wakati na upungufu wa vifaa tiba katika hospitali wilayani Kahama.

Aidha ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikitumia rasimali nyingi kuhakikisha kuna upatikanaji wa dawa za kutosha.
Pia kumekuwepo upotevu wa dawa unaosababishwa na baadhi ya watumishi wasio kuwa waaminifu kwa kutofuata mifumo iliyopo au kuweka taarifa vizuri hivyo kuwataka kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuweka sawa taarifa ya matumizi ya vifaa tiba.

Dkt. Subi ameongeza kuwa kimsingi Idara yake inaangazia sana utoaji elimu ya Afya kwa wananchi kwani elimu ya Afya ndio msingi wa huduma za kinga hapa Nchini akitolea mfano Wilaya ya Kahama kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI.

‘’Wilaya ya Kahama ina jumla ya wagonjwa 15,000 wanaotumia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI idadi hii ni kubwa sana lakini tukitoa elimu ya UKIMWI idadi hii inaweza kupungua kwa kiasi kikubwa sana na kuokoa fedha nyingi za serikali zinazotumika kununua dawa za ARV,’’ aliongeza Subi.

Pamoja na masuala mengine yanayoshughulikiwa na idara ya Kinga ya Wizara ya Afya Dkt. Subi ameongeza kuwa Idara yake pia inashughulikia masuala ya lishe suala ambalo kimsingi ni la utoaji elimu kwa umma na kuoji kuwa kwanini bado kuna udumavu katika jamii zetu kwani Tanzania ni Nchi inayozalisha Chakula cha kutosha na kusema kuwa sio tu watoto wana udumavu wa kimo pia wanachangamoto ya udumavu wa akili.

Naye Mkurugenzi wa Mji wa Kahama, Anderson Msumba amesema kuwa kwa upande wake ameona mapungufu yaliyobainishwa na ukaguzi shirikishi na kuhaidi kuyafanyia kazi kwa kipindi kifupi yale amabayo hayaitaji fedha laikini pia yale yanayoitaji rasilimali fedha atayafanyia kazi kabla ya Desemba Mwaka huu.

Idara ya Kinga ya Wizara ya Afya inaendelea na kazi ya ukaguzi wa miundombinu ya Hospitali kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Geita, Mara na Kagera.
Picha mbalimbali zikimuonyesha Dk Subi wakati wa ziara yake mjini Kahama.