Header Ads Widget

STEVEN MACHUMU ATIA NIA UBUNGE CCM MUSOMA VIJIJINI KUMPIMA PROFESA MHONGO


Mtia nia ya ubunge Jimbo la Musoma Vijijini kwa tiketi ya CCM, Steven Tumaini Machumu.

Na Mwandishi Wetu–Shinyanga Press Club Blog

NI Dhahiri! majina makubwa na mashuhuri yakiwemo ya wasomi wakubwa nchini yanayotajwa kuutaka ubunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Mkoani Mara, hayawatishi wala kuwazuia raia wengine wa kawaida wenye nia ya dhati ya kuliwakilisha jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hii ni baada ya Mwanaharakati wa Maendeleo jimboni humo, Steven Machumu kuingiza miguu yake kwenye vita ya kusaka nafasi ya kuwawakilisha wananchi wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM.

Machumu ambaye ni mwanaharakati wa maendeleo na mikakati mbalimbali ya kupunguza umaskini jimboni humo kwa miaka nane sasa, ametangaza nia ya kugombea ubunge huo kupimana ubavu na Profesa Sospeter Mhongo anayetetea nafasi hiyo pamoja na majina mengine makubwa ya wasomi wakiwemo maprofesa wanaotajwa kwa sasa.

Machumu
Machumu ambaye ni Mwenyekiti wa Nyanja Economic Investment Trust Fund (NEIT) inayotekeleza miradi yake katika wilaya za Musoma na Rorya, ametangaza nia yake hiyo Julai 9, 2020 mjini Shinyanga wakati akizungumza na Shinyanga Press Club Blog, na kueleza kuwa ndiye mwenye nia ya dhati ya kuwasaidia wananchi wa jimbo hilo waliogubikwa na umaskini kwani amekuwa akifanya hivyo kwa muda mrefu sasa kuliko wanasiasa wengine ambao wanakwenda kutafuta ajira za kisiasa.

Amesema kwa sasa ni kama jimbo hilo limepoteza dira na hakuna mwanasiasa mwenye mkakati wa dhati kulikomboa na umaskini, tofauti na yeye ambaye mwaka 2013 alikuja na mkakati kupitia andiko lililopitishwa na baraza la madiwani wa halmashauri ya Musoma Vijijini kama mradi wa maendeleo, ambapo baadae walifanikiwa kuanzisha vikundi vya kusaidia kupunguza umaskini.

Ameenda mbali na kubainisha kuwa endapo atafanikiwa kuipeperusha bendera ya CCM basi kipaumbele chake jimb oni humo kitakuwa ni elimu, uwekezaji na akiba na kujenga dira ya jimbo kwani ndivyo msingi wa maendeleo ya jamii ikizingatiwa kwamba jimbo hilo halina uwekezaji binafsi.

“Nina wiwa kwa mapana na ujasiri mkubwa kutokana na harakati mbalimbali za kimaendeleo katika jimbo letu nilizozitekeleza, nina utofauti na wanasiasa wengi wanaouhitaji ubunge kwa sababu nikiona msururu wa hao watia nia wengi wanataka ajira za kisiasa lakini hakuna Mwana Musoma Vijijini asiyetambua juhudi zangu za kuwaletea maendeleo.

“Ninajivunia rekodi kubwa ya mambo ambayo nimeyafanya tofauti na wenzangu wanaokwenda bila chochote, katika harakati hizi nimethibitisha kwa dhati kwa vitendo na ushahidi mkubwa katika jamii yangu.  Ni mtu wa kwanza niliyetoa semina elekezi ya kuwasaidia wakulima zaidi ya 300 kwenye jimbo hilo ili kufanya kilimo bora chenye tija na uzalishaji mkubwa na tulifanikisha kupata mifuko 600 ya mbole kutoka Minjingu,” alisema.

Machumu anajivunia juhudi zake zilizowezesha kupeleka wafadhili kuomba shamba la Bugwema, kufanya tathmini ya wajane, yatima, wazee wasiojiweza na watu wenye ulemavu ambapo takribani watu 5,000 wako kwenye mpango wa kusaidiwa.

Pia ameisaidia jamii ya Musoma vijijini kwa kilimo biashara kupitia program ya elimu ya fedha na ujasiriamali, kuanzisha program ya kusaidia elimu ya msingi na dhana za kilimo kwa kushirikiana na wadau, ambapo ameandika vitabu saba ikiwemo kuboresha elimu, kutambua changamoto za kimaendeleo jimboni humo na kwamba hakufanya kwa nia ya kutafuta umaarufu bali nia ya dhati ya kuwainua wananchi.

“Nimekuwa karibu nao kwa sababu hakuna mwanasiasa mwenye nia ya dhati ya kulikomboa jimbo letu na janga la umaskini, lakini mimi baada ya jitihada zote hizo nilibaini kwamba watu hawana mitaji nikatembelea baadhi ya benki nikaja na mpango mkakati wa kufungua huduma ya kibenki kila kata jimboni humo (Rural Financial Bank Outlet) ambao umeanza utekelezaji,” alisema.

 Machumu alipofika bungeni kuwasilisha mikakati yake ya kuwasaidia wananchi
 Sehemu ya kikundi cha kupunguza umaskini jimboni humo kilichoanzishwa na Machumu 
 Baadhi ya watoto yatima, wajane na watu wenye ulemavu kutoka jimboni humo walio kwenye mpango wa kusaidiwa kupitia juhudi za Machumu wakiwa katika picha ya pamoja nje ya jengo la pamoja Jijini Dodoma
Machumu akiwa katika majukumu yake
 Sehemu ya vikundi vilivyoko kwenye mpango mkakati wa kuanzisha huduma za kibenki katika kila kata jimboni humo vilivyoanzishwa na mwanaharakati huyo