Header Ads Widget

MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YATAKIWA KUENDESHA MIRADI YENYE TIJA KWA WANANCHI

 Wanufaika wa miradi ya kilimo na ufugaji katika vijiji vya Kipanga na Ilogombe wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Dkt. Faustine Sambaiga katika kikao cha pamoja alipotembelea vijiji hivyo kukagua miradi inayotekelezwa na shirika la PELUM Tanzania.

 Na Mwandishi wetu -Mufindi
Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Dkt. Richard Sambaiga ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kuhakikisha miradi wanayoifanya inawaongezea tija wananchi badala ya kufadhili miradi isiyoweza kuleta maendeleo kwa walengwa.

Dkt. Sambaiga ameyasema hayo wilayani Mufindi mkoa wa Iringa wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya kilimo, ufugaji na mpango wa matumizi bora ya  ardhi inayofanywa na Shirika la PELUM Tanzania katika vijiji vya Kipanga na Lilongole.

"Kuna umuhimu kwa hawa wananchi wanaofanya kilimo au ufugaji  wafanye kwa namna ambayo itawaongezea tija, kuliko kuona wanatumia nguvu nyingi lakini tija kidogo" amesema Dkt. Sambaiga.

Amesisitiza mwenendo wa mashirika kuripoti kazi walizofanya na kufanikiwa, ziendane na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi ili miradi hiyo iwe mfano na kuhamasisha wengine kujiunga. 

"Tuongeze vipengele vya kuwezesha utaalamu wa kilimo na ufugaji uwe wa kisasa ili kuongeza tija na miradi hiyo iwe ni mfano"

Naye Msajili wa Mashirika yasiyo Ya Kiserikali,  Vickness Mayao ameyataka mashirika hayo kutoa taarifa mara kwa mara kwa wananchi kuhusu kazi zao na kuboresha majukumu wanayoyafanya. 

"Bado tunahimiza mashirika kutekeleza majukumu yao kwenye eneo walilosajili, wanaweza kuongeza thamani ya miradi yao bila kuathiri lengo lao" amesema Mayao.

Akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Mratibu wa shirika hilo Donati Senzia amesema, shirika kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, inatarajia kupima mashamba zaidi ya 500 ili wananchi hao wapewe hati na ardhi ili kuwanufaisha kiuchumi.

"Tuliona kwenye mradi huu tusiishie tu kupima bali tuangalie ardhi itawanufaishaje wananchi kiuchumi hasa kwa akina mama" amesema Senzia. 

Naye Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Simon Mbago amesema wanashirikiana na mashirika mbalimbali kuhakikisha wananchi wananufaika na ardhi kwa kuwapimia na kubainisha matumizi ya ardhi.

Baadhi ya wanufaika wa vijiji hivyo wameelezea kufurahishwa kwao na PELUM hususani kupata elimu ya kumiliki na kuitumia ardhi kwa manufaa na kupunguza migogoro ya ardhi kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo, wananchi wengi waliomba Serikali kwa kushirikiana na NGOs kuwasaidia kutatua kero ya Barabara na maji ili kuwawezesha kujikita katika Kilimo.

"Kipaumbele kwetu ni barabara kwani hata haya mazao hatuwezi kuyafikisha kwenye masoko barabara yetu inapitika katika msimu mmoja tu, wakati wa mvua hatuwezi kufika mjini", alisema mmoja wa wanakijiji. 

Ziara ya ukaguzi wa kazi za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali inakusudia katika kujirishisha dhidi ya taarifa za Mashirika zinazowasilishwa katika Ofisi ya Msajili, taarifa za wafadhili pamoja na kujiridhisha na thamani halisi ya fedha zilizotumika katika maeneo ya mradi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Dkt. Faustine Sambaiga akizungumza na wanakijiji wa Ilogombe, Wilaya ya Mufindi katika kikao cha pamoja na wanufaika wa miradi ya kilimo na mifugo inayotekelezwa na shirika la PELUM Tanzania.
Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Dkt. Faustine Sambaiga akiangalia ubao unaoonesha upimaji wa maeneo na matumizi ya ardhi katika kijiji cha Kipanga Wilayani Mufindi.

Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW