Header Ads Widget

FAMILIA 30 ZA WAATHIRIKA WA UKATILI PEMBA, ZAPEWA KUKU 300

Mratibu wa TAMWA Zanzibar Ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said akimkabidhi Kuku mmoja wa wahanga wa utelekezaji Wilaya ya Wete  ikiwa ni miongoni mwa juhudi za TAMWA Zanzibar kuwawezesha wanawake hao kujisimamia kiuchumi.

Na Gaspary Charles- TAMWA Zanzibar
FAMILIA za waathirika wa vitendo vya udhalilishaji kisiwani Pemba wameshukuru na kupongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-Zanzibar za kupambana na vitendo vya udhalilishaji katika jamii.

Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ya wanafamilia hao mara baada ya kukabidhiwa Kuku na chama hicho kwaaajili ya uguaji ikiwa ni sehemu ya juhudi za chama hicho kupambana na vitendo vya udhalilishaji.

Mmoja wa wanufaika wa msaada huo Bi Mpemba Ali Moh’d amesema Kuku hao watawasaidia kujiendeleza kiuchumi kulingana na hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo.

“Tunawashukuru sana watu wa TAMWA kwa kutambua matatizo yetu na kuamua kutuletea msaada huu wa Kuku kama sehemu ya faraja kwetu, tunajisikia furaha sana kwakweli leo,” alisema.

Aidha ameongeza kuwa kutokana na familia hizo kuwa katika hali ngumu ya maisha kupitia ufugaji wa Kuku itawawezesha kurahisisha upatikanaji wa huduma za msingi katika familia zao.

“Kupitia Kuku hawa tuliopewa leo watatusaidia sana kututalulia shida nyingi majumbani mwetu kama vile chakula kulingana na hali zetu ndio kama hivo hatujiwezi na hatuna shughuli nyingine yoyote ya kutupatia kipato,” alisema Mpemba.

Kwa upande wake Shaali Makame Sahaali amesema licha ya Kuku hao kuwasaidia kujiendeleza kiuchumi lakini pia imechochea hamasa kwa familia hizo kujiona kuwa sehemu ya jamii kulingana na hali zao.

“Niseme tu kwamba TAMWA imefanya jambo kubwa sana leo kwani licha ya mitihani tuliyokumbana nayo lakini kupitia hili nasisi tumefarijika sana na kujiona kuwa sehemu ya jamii,” alisema.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, katibu wa Sheha ya Kiwani Wilaya ya Mkoani, Mohamed Haji Suleiman alishukuru mchango wa TAMWA Zanzibar katika kulinda na kutetea haki za kijamii Zanzibar na kukitaka chama hicho kuendelea na juhudi hizo ili kuhakikisha jamii inabaki salama.
  
“Juhudi hizi zinazoendelea kuchukuliwa na TAMWA si kazi ndogo. Niwaombe sana endeleeni na juhudi hizi ili kuhakikisha mnasaidia kutokomeza vitendo vyote vya udhalilishaji katika jamii zetu Zanzibar,” alisema.

Mapema mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said amesema lengo la kutoa msaada wa Kuku kwa familia za wahanga wa vitendo vya udhalilishaji ni kuwawezesha kuwa na shughuli za kujiingiza kipato katika familia.

“Tumeamua kutoa msaada huu kwa familia hizi ili uwasaidie kuendeshwa familia zao kutokana na wengi wao kuwa katika hali ngumu ya maisha,” alisema.

Aidha mratibu huyo ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kupinga udhalilishaji Zanzibar katika kuwawezesha wahanga kujihusisha na shughuli za uzalishaji ili kuwa na uwezo wa kufuatilia kesi zao mahakamani.

Alisema, “miongoni mwa malengo ya kutolewa kwa Kuku hawa ni kuwawezesha kupata shughuli ambayo itawasaidia kupata kipato cha kufuatilia kesi zenu ili muweze kupata haki zenu.”

Jumla ya Kuku 300 wamegawiwa kwa familia 30 za wahanga wa vitendo hivyo kutoka Wilaya ya Mkoani na Wete Pemba.
Afisa Masoko kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
TAMWA Zanzibar, Muhidin Ramadhan akimkabidhi Kuku mmoja wa wahanga wa Utelekezaji Wilaya ya Mkoani.

Mratibu wa TAMWA Zanzibar Ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said  akikabidhi Kuku kwa  familia za wahanga wa vitendo vya udhalilishaji katika Ofisi za TAMWA Pemba.

Mratibu wa TAMWA Zanzibar Ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said akimkabidhi Kuku Mpemba Ali Moh’d wakati wa zoezi la Utoaji wa Kuku kwa wahanga wa Utelekezwaji Wilaya ya Mkoani Pemba.  

Mratibu wa TAMWA Zanzibar Ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said akikabidhi chakula cha Kuku kwa mmoja wa wahanga wa Utelekezaji mara baada ya kukabidhiwa Kuku mapema leo Julai 22 huko Ofisi za TAMWA Pemba.