Header Ads Widget

AHMED: NIMEFANYIWA MENGI LAKINI SASA NIMESAMEHE KILA KITU, TUSONGE MBELE


Ahmed Salum

Na Damian Masyenene –Shinyanga Press Club Blog
Baada ya ushindi wa kura 377 za maoni dhidi ya 304 za mpinzani wake wa karibu kwenye kinyang’anyiro cha kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuteuliwa kugombea ubunge wa Jimbo la Solwa (Shinyanga Vijijini) mkoani Shinyanga, Ahmed Salum amesema sasa anasamehe vitendo vyote alivyofanyiwa wakati wa mchakato huo na ameamua kusonga mbele, huku akijinasibu kuwa uwezo wa kupmbana na wagombea wa vyama vya upinzani anao.

Ahmed ambaye ni mgombea anayetetea kiti cha ubunge wa jimbo hilo baada ya kuliongoza kwa miaka 15, ametoa kauli hiyo leo Julai 20, 2020 kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, mjini Shinyanga wakati akitoa neno la shukrani kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Vijijini baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kura za maoni.

Mwanasiasa huyo amesema kuwa endapo jina lake litateuliwa na CCM basi anaahidi ushirikiano kwani hana kinyongo japokuwa anafahamu vita ilikuwa kubwa sana, ambapo amewaomba wana CCM wote wakiwemo watia nia wenzake kuvunja makambi (makundi) na kusonga mbele kwa manufaa ya chama hicho.

“Sina kinyongo, nafahamu vita ilikuwa kubwa sana lakini naomba tuvunje makundi nimesamehe yote na kwa yeyote aliyenikwaza nimemsaheme….uwezo wa kupambana na wagombea wa upinzani ninao kwahiyo tuendelee kushirkiana,” amesema.

Naye mshindi wa pili katika kura hizo za maoni, Azza Hilal amesema kuwa wajumbe (wapiga kura) wametenda kile kilichostahili kwa kila mgombea, hivyo akawaomba wagombea wenzake kusonga mbele na kuyazika yale yote yalitokea nyuma.

“Niwaombe wagombea wenzangu hili limekwisha hakuna cha ‘Team Azzah’ ama nani bali hii ni timu CCM, nawashukuru kwa kura mlizonipa hii ni heshima kwangu,” amesema Azza.

Akitoa neno kwa niaba ya watia nia wengine 52, Mzee Sprian Mnyedu amewapongeza wenzake kwa uvumilivu mkubwa waliounyesha na kuhakikisha zoezi hilo linamalizika salama, na kuwataka wenzake kuungana ili Solwa isonge mbele na kupiga hatua za maendeleo.

“Nashukuru Mungu kwa zoezi hili kumalizika salama bila mihemko, tukubali kwamba mambo yameisha na tuwe marafiki, aliyeshinda tunampongeza kile alichokipata ni maamuzi ya wanachama na tunakiheshimu,” amesema.