Header Ads Widget

CHAMA CHA UPINZANI NCHINI MALAWI CHAONGOZA KURA ZA MARUDIO URAIS ZINAZOHESABIWA




















Kiongozi wa chama cha Malawi Congress (MCP) Lazarus Chakwera ndiye kinara wa muungano wa upinzani

Upinzani nchini Malawi unaelekea kupata ushindi katika kura ya uchaguzi wa urais inayofanyiwa marudio baada ya matokeo yake kufutiliwa mbali kufuatia madai mengi ya udanganyifu.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huo uliofanyika siku ya Jumanne hayajatangazwa na tume ya uchaguzi ya Malawi.

lakini chombo cha habari cha serikali MBC kinasema kwamba kiongozi wa upinzani Lazarus Chakwera anaongoza na asilimia 59 ya kura zilizohesabiwa.

Rais Peter Mutharika , ambaye anawania muhula wa pili ana asilimia 38 ya kura zilizohesabiwa, kinasema.

Mgombea wa tatu ambaye hakuonekana kama mgombea mkuu Peter Kuwani anasemekana kujiapatia asilimia 2 ya kura hizo.

Mwaka uliopita, Malawi ilikuwa nchi ya pili barani Afrika kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais kufuatia madai ya udanganyifu, baada ya Kenya 2017.

Mwandishi wa BBC katika eneo la kusini mwa Afrika, Andrew Harding anasema sio jambo la kawaida na kwa wengi linavutia - Mahakama iliingilia kati na kubadilisha matokeo katika eneo ambalo wizi wa kura ni suala la nyeti.

Muongozo wa uchaguzi wa Malawi

Wafuasi wa bwana Chakwera tayari wameanza kusherehekea kile wanachoamini ni ushindi wa kihistoria - katika kile kinachoaminika kuwa tukio la kwanza katika eneo la sahara kwamba uchaguzi uliokumbwa na udanganyifu umebadilishwa na upinzani kuibuka na ushindi ukichukua madaraka kwa njia ya kidemokrasia.

Pongezi pia zimetolewa na viongozi wa upinzani katika mataifa ya Afrika ya kusini.

"Maisha mapya kwa Malawi!," alisema kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Nelson Chamisa.

"Mungu ameipatia Malawi Mcha Mungu'', aliongezea akitaja historia ya Chakwera kama kiongozi wa dini.

''Ndugu yangu, rafiki yangu na kiongozi ameshinda uchaguzi wa Malawi. Niliwasiliana naye kwa simu na kusherehekea ushindi wake'', alituma ujumbe wa twitter kiongozi wa zamani wa chama cha upinzani cha DA Mmusi Maimane.

Subira iliojaa wasiwasi

Mwandishi wa BBC anasema taasisi za kidemokrasia nchini Malawi huenda zikakabiliwa na shinikizo kali katika saa chache na siku zijazo.

Taifa hilo lilikuwa limegawanyika kabla ya uchaguzi huo wa marudio huku kukiwa na maandamano makubwa ya kupinga serikali.

Kiongozi mkuu wa serikali amedaiwa kusema kwamba uchaguzi unaibiwa.


Watu walipiga kura Jumanne licha ya hofu ya coronavirus

Akizungumza siku ya Jumanne baada ya kupiga kura kusini mwa Malawi, bwana Mutharika alidai kumekuwa na ghasia katika maeneo ya upinzani, kilisema chombo cha habari cha Reuters.

''Inasikitisha. katibu wetu mkuu amepigwa . wale wanaosababisha ghasia hawana la kufanya '', Reuters ilimnukuu rais akisema.


''Ni vipi sasa kwamba uchaguzi huu utakuwa wa haki na huru''?, aliuliza.


Hata hivyo ripoti hizo hazijathibitishwa.