
Na Salvatory Ntandu - Ushetu
Katika jitihada za kupambana na Ugonjwa wa homa kali ya Mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona, Kanisa la Kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya kusini Mashariki ya ziwa Victoria limetoa Msaada wa vifaa vya kujikinga dhidi ya COVID 19 kwa waganga wa tiba asili vyenye thamani ya shilingi Milioni 3.5.
Akizungumza katika hafla maalum ya kukabidhi vifaa hivyo Jana na Askofu wa Dayosisi hiyo Dkt, Emmanuel Joseph Makala kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu Michael Matomora alisema kuwa, Kanisa limetoa vifaa hivyo kwa waganga hao ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa huo katika maeneo yao ya kazi.
Alisema ,Kanisa limebaini kuwa waganga wa tiba asili, wanafanya kazi katika mazingira hatarishi kutokana na kuhudumia wateja wao bila ya kuwa na vifaa maalumu vya kujikinga na ugonjwa wa COVID 19 kama vile vitakasa mikono, ndoo za maji na barakoa.
“Kundi hili ni Muhimu hivyo,kanisa limeamua kuwajali kwa kutoa vifaa hivi katika mikoa mbalimbali ya kanda ya ziwa kwa kuanza na Bariadi mkoa wa Simiyu na Ushetu mkoa wa Shinyanga ili ,kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu”,alisema Dkt Makala.
Awali akipokea vifaa hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Michael Matomora alilishukuru kanisa la KKKT kwa kutoa vifaa hivyo ambavyo vitatumika na waganga wa jadi na vingine vitapelekwa katika kituo cha afya Ukume ili kuwa kinga wagonjwa wanaokwenda kupata huduma katika maeneo hayo.
Alifafanua kuwa Ofisi yake itahakikisha vifaa hivyo vinawafikia waganga wote wa tiba asili sambamba na kuyaomba mashirika mengine kuiga mfano wa kanisa la KKKT kwa kuendelea kutoa vifaa vya kujikinga na COVID 19.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa waganga wa Tiba Asili katika Halmashauri hiyo, Shumileta Charles alisema wanaendelea kuzingatia maelekezo ya serikali katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na wanahakikisha kabla ya kutoa huduma wateja wao wananawa mikono na kuvaa barakoa.
“vifaa hivi vilivyotolewa na kanisa vitasaidia kuwakinga waganga wa tiba asili dhidi ya janga la Corona na nichukue fursa hii kupitia vyombo vya habari kuwataka wazingatie maelekezo ya serikali ili kujikinga wao na pindi wanapokuwa wanawahudumia wateja wao,”alisema Charles.