Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, ametembelea kituo cha Taasisi ya Forodha ya Korea Kusini katika mji wa Daejeon, nchini Korea Kusini, kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi na upatikanaji wa mifumo ya forodha wakati wote ili kurahisisha utoaji wa huduma.Katika ziara hiyo, Bw. Mwenda amepata fursa ya kujifunza namna Taasisi hiyo inavyohakikisha mifumo yake ya forodha inakuwa imara, inapatikana muda wote na inafanya kazi kwa ufanisi, hatua inayowezesha kurahisisha taratibu za forodha na kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wafanyabiashara na wadau wengine.
Aidha, ziara hiyo imekuwa fursa ya kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu za kuimarisha miundombinu ya TEHAMA, kuhakikisha mifumo inakuwa endelevu na kupunguza changamoto zinazoweza kusababisha kukwama kwa huduma za forodha. Uzoefu huo ni muhimu katika kuendeleza ufanisi wa mifumo ya TANCIS na IDRAS inayotumiwa na TRA.
Kupitia ziara hiyo, TRA inalenga kupata maarifa na uzoefu utakaosaidia kuimarisha mifumo yake ya forodha, kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wakati wote na kurahisisha taratibu za forodha, hatua itakayochangia kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza ufanisi wa shughuli za forodha na kuridhisha walipakodi.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464



