Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Paul Chacha, ambaye pia ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Idara ya Oganaizesheni, amefanya ziara mkoani humo huku akiwataka wana CCM kupinga vitendo vya rushwa, makundi na kupanga safu za uongozi.
Amefanya ziara hiyo leo Novemba 7,2026 pamoja na mambo mengine pia alisimikwa na wazee wa kimila na kupewa cheo cha Nsumba Ntale na jina la Limbe Ndulu ya Makubi.
Akizungumza na Kamati ya Siasa pamoja na Halmashauri Kuu ya CCM mkoani humo, amesema, iwapo chama kitaepuka vitendo hivyo, kitaendelea kuwa imara sababu ndiyo vitu ambavyo vimekuwa vikiwavuruga, huku akiwataka wanachama hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujenga uchumi imara wa chama.
"WanaCCM tuepuke vitu vitatu tu, rushwa, makundi, na kupanga safu za viongozi hayo ndiyo yanatuvuruga," amesema Chacha.
Katika hatua nyingine amesema, nchi ya Tanzania ni nchi yenye raha na imepiga hatua kubwa kimaendeleo na kuwashangaa wanaobeza maendeleo hayo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, akizungumza kwa niaba ya wabunge wa mkoa huo, amesema watafanyia kazi na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na mlezi wao kwa lengo la kukiimarisha chama hicho.
Aidha, katika ziara hiyo pamoja na mambo mengine, pia aligawa baiskeli 30 za watu wenye ulemavu zilizotolewa na Mbunge Patrobas Katambi na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi.
TAZAMA PICHA👇👇
Mlezi wa CCM Mkoa wa Shinyanga Paul Chacha akizungumza.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa akizungumza.
Mbunge wa Shinyanga Mjini Patrobas Katambi na Waziri wa Mambo ya Ndani akizungumza.
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Sophia Kibaba akizungumza.