Na Rose Ngunangwa, Dar es Salaam
Kwaya ya Mtakatifu Joseph kutoka Parokia ya Bikira Maria wa Mlima wa Karmeli (Bunju), mwishoni mwa wiki ilikonga nyoyo za wapenzi wa muziki mtakatifu baada ya kutumbuiza kwa ustadi mkubwa wakati wa tamasha lao maarufu kama St. Joseph Music Gala 2026.
Tamasha hilo la aina yake lilivuta hisia kubwa miongoni mwa wahudhuriaji, kwani wanakwaya hao waliimba jumla ya nyimbo 47 zenye mahadhi mbalimbali, zikiwemo za zamani na nyingine za Kiitaliano.
Akizungumza baada ya tamasha hilo, mmoja wa marafiki wa kwaya hiyo, dada Sara Tenywa, alisema, “Kwa kweli tumetoka tukiwa wapya, vijana wameimba.”
Kwa upande wake, Rehema Mayemba, ambaye alifuatilia tamasha hilo kupitia mtandaoni, alitoa pongezi zake akisema, “Hongereni kwa muziki mtakatifu. Aisee imekuwa nzuri sana, nimependa. Tuombe uzima wakati mwingine nitashiriki.”
Naye mmoja wa marafiki waliohudhuria tamasha hilo alieleza kufurahishwa kwake akisema kwamba ameburudika sana na uimbaji huo kiasi cha kusahau kama kuna kufa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Askofu (Vicar General) wa Watawa wa Kiume katika Jimbo la Bagamoyo, Padre Dominic Somola (OCarm), aliwapongeza wanakwaya hao kwa uwezo na pumzi waliyoonyesha, na kuahidi kuwasaidia kufikia malengo yao kadri Mungu atakavyomjalia.
Padre Somola, ambaye pia ni Paroko wa parokia hiyo, aliwasilisha salamu za Baba Askofu wa Jimbo la Bagamoyo, Mhashamu Stephano Msomba, ambaye alikuwa mgeni rasmi na kuwakilishwa naye katika tamasha hilo.
Katika miaka ya hivi karibuni, Kwaya ya Mtakatifu Joseph kutoka Bunju imejizolea umaarufu mkubwa kutokana na uimbaji wake wa viwango vya juu chini ya uongozi wa mwalimu Antipas Chuwa, ambaye wengi hupenda kumuita “Jose Mourinho” au “The Special One” kutokana na umahiri wake mkubwa wa kukipanga na kukipika kikosi vema.
Katika tamasha hilo, kwaya iliingia jukwaani kwa awamu tatu na kuimba nyimbo za zamani za Kikatoliki, nyimbo zinazovuma kwa sasa kama Tegemeo Letu na Mimi Mkatoliki, pamoja na nyimbo zilizomo kwenye albamu zao kama vile Ona.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464




