` BARRICK NORTH MARA YAZINDUA WIKI YA KUIMARISHA MAHUSIANO NA JAMII INAYOZUNGUKA MGODI

WANDAMAN HOTEL

BARRICK NORTH MARA YAZINDUA WIKI YA KUIMARISHA MAHUSIANO NA JAMII INAYOZUNGUKA MGODI

    


Baadhi ya washiriki wakishiriki mbio za kilomita tatu wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Mahusiano ya Mgodi wa Barrick North Mara, uliofanyika Nyamongo, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Mahusiano katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ingwe, Nyamongo, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara. 
Meneja wa Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick North Mara, Franscis Uhadi, akizungumza na wafanyakazi na wananchi wa Nyamongo wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Mahusiano, itakayohusisha michezo mbalimbali kwa lengo la kuimarisha afya, mshikamano na mahusiano kati ya mgodi na jamii inayouzunguka.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Stephen Doyle, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Mahusiano katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ingwe, Nyamongo, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC), Diwani Rashid Bugomba, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Mahusiano ya Mgodi wa Barrick North Mara, uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ingwe, Nyamongo, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

#Itahusisha michezo na elimu kwa jamii kuhusu athari za uvamizi wa mgodi

**
Na Mwandishi Wetu, Nyamongo, Tarime

Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara umezindua rasmi Wiki ya Mahusiano, itakayohusisha michezo mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ushirikishwaji wa vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo, kukuza maelewano na kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo.

Wiki hiyo pia itatumika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli za mgodi na athari za vijana kujihusisha na vitendo vya uvamizi wa maeneo ya uchimbaji (intruders), ambavyo vinaweza kuathiri uzalishaji, mapato ya halmashauri, wilaya, mkoa na taifa, pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Mpango huo, ambao awali ulijulikana kupitia mashindano ya soka ya vijana ya kuwania Kombe la Mahusiano, sasa unatoa fursa pana zaidi ya kuwaunganisha viongozi na wafanyakazi wa mgodi pamoja na wananchi kupitia michezo na shughuli nyingine za kijamii.

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumamosi katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ingwe, vilivyopo kilomita chache kutoka mgodini, katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Wiki hiyo itashirikisha vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo, ambapo wananchi watapata fursa ya kushiriki michezo mbalimbali pamoja na mbio za jogging zitakazolenga kuimarisha afya za wafanyakazi, vijana, wanawake na jamii kwa ujumla.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mkuu wa Barrick North Mara, Stephen Doyle, amesema mpango huo ni muhimu katika kujenga maelewano na mazungumzo kati ya mgodi na jamii, kusikiliza changamoto za wananchi na kushirikiana kutafuta suluhisho.

“Nachukua nafasi hii kumshukuru Mkuu wa Wilaya na viongozi wote wa wilaya na Halmashauri ya Tarime kwa kuja kutuunga mkono katika wiki hii muhimu, ambayo ni sehemu ya juhudi zetu za kuimarisha mahusiano na jamii inayozunguka mgodi,” alisema Doyle.

Alisema mawasiliano kati ya mgodi na vijiji 11 vinavyouzunguka ni hatua muhimu katika kuongeza ufanisi wa shughuli za uchimbaji na uzalishaji wa madini katika eneo hilo.

Alibainisha kuwa, mbali na kuimarisha afya za washiriki, michezo ni nyenzo muhimu ya kujenga mshikamano na kukuza mahusiano kati ya jamii na mgodi.
“Wiki hii inafungua fursa kwa viongozi na uongozi wa mgodi kujadili namna ya kuishi kwa amani na vijiji hivi 11, kueleweshana kuhusu shughuli za mgodi na manufaa yake kwa jamii, mkoa na taifa. Pia itawawezesha wananchi kuelewa umuhimu wa kanuni na sera za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) na manufaa yake,” aliongeza.

Doyle alisema michezo pia huchochea ajira, kipato na maendeleo ya mtu binafsi, hivyo kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo kushiriki kikamilifu katika shughuli zilizoandaliwa.

Alifafanua kuwa mgodi huo umepokea ombi la Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) la kujenga uwanja wa mpira na tayari umenunua eneo kwa ajili ya mradi huo. Hata hivyo, hatua ya kupata hati ya eneo hilo bado inaendelea kabla ya kuanza kwa ujenzi.

Aidha, aliwataka viongozi, wazazi na wakazi wa Nyamongo kushirikiana kutoa elimu kwa vijana kuhusu athari za uvamizi wa maeneo ya mgodi, akisema vitendo hivyo vimeanza kujitokeza tena kwa wingi.

Alisema kuingia ndani ya eneo la mgodi kwa lengo la kuchimba dhahabu bila ruhusa ni kitendo kinachoweza kuhatarisha shughuli za uchimbaji na uzalishaji.
“Vitendo vya uvamizi katika maeneo ya mgodi wetu vitaathiri uzalishaji na kusababisha kukosekana kwa mapato kwa halmashauri, wilaya, mkoa na taifa kutokana na shughuli za uchimbaji katika maeneo yenye leseni ya North Mara,” alisema.

Aliongeza kuwa vitendo hivyo vinaweza pia kuathiri upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, alisema Wiki ya Mahusiano ni sehemu ya kuwaunganisha wananchi wa Nyamongo kupitia michezo inayolenga kuimarisha afya, mshikamano na usalama wa jamii.

“Uzinduzi huu wa Wiki ya Mahusiano kwa Jamii ni muhimu na tukio kubwa la kuwaunganisha watu pamoja na kukuza maelewano na ushirikiano kupitia vijiji vyote 11,” alisema.

Meja Gowele aliongeza kuwa mpango huo utaimarisha ushirikiano kati ya mgodi na wakazi wa maeneo yanayouzunguka, huku ukichochea mshikamano ili uwekezaji huo uwe na manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Alisema uvamizi katika maeneo yenye leseni ya uchimbaji ya Barrick North Mara hauwezi kukubalika kwa kuwa unaweza kuvuruga shughuli za kila siku za mgodi na kupunguza uzalishaji wa dhahabu.

Alibainisha kuwa kupitia sera na kanuni za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), mgodi umetekeleza na unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na miundombinu, pamoja na kuchochea mnyororo wa thamani na uanzishwaji wa viwanda.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC), Diwani Rashid Bugomba, alisema mpango huo ni daraja muhimu la kuwaunganisha wananchi wa Nyamongo na vitongoji vyake na mgodi wa Barrick North Mara kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote.

Bugomba alizitaka vijiji vyote 11 kushiriki kikamilifu katika shughuli za wiki hiyo, akieleza kuwa michezo mbalimbali, ikiwemo Mahusiano Cup, ni fursa ya kuimarisha afya na mshikamano wa wananchi.
Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick North Mara, Franscis Uhadi, alisema wiki hiyo itatoa fursa kwa wafanyakazi na wananchi wa vijiji vyote 11 kushiriki michezo mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha afya zao na kujenga mahusiano.

Alisema mpango huo pia utasaidia kuwapa wananchi uelewa kuhusu shughuli za mgodi, manufaa yake kwa jamii na utekelezaji wa sera na kanuni za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), zinazowezesha miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Kutakuwa na michezo na mashindano mbalimbali, ambapo washindi watapata zawadi. Pia tutatembelea vijiji vyote 11 vinavyozunguka mgodi wetu kwa ajili ya kutoa elimu na kuimarisha mahusiano,” alisema.

Katika uzinduzi huo, viongozi wa mgodi wa Barrick North Mara, Mkuu wa Wilaya ya Tarime na viongozi wa Halmashauri ya Tarime walishiriki mbio fupi za jogging.

Katika kipindi cha Wiki ya Mahusiano, wananchi wa Nyamongo na vitongoji vyake watashiriki michezo mbalimbali, ikiwemo mpira wa miguu. Miongoni mwa michezo iliyoandaliwa ni mechi kati ya Nyamongo FC na Tarime FC, itakayochezwa Jumapili ya wiki ijayo.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464