Afisa Mahusiano ya jamii wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo akikabidhi begi kwa mmoja wa wanafunzi wanufaika.
Sehemu ya mabegi yaliyotolewa na Barrick
Picha ya pamoja za wafanyakazi kazi wa Barrick na Wanafunzi na walimu wao.
Picha ya pamoja za wafanyakazi kazi wa Barrick na wanafunzi na walimu wao.
Wanafunzi wakifurahia zawadi walizokabidhiwa.
***
Wakati dunia ikielekea kuadhimisha Siku ya Mtoto Duniani wiki hii, yenye kauli mbiu isemayo “Siku yangu. Haki zangu. Mustakabali Wangu” Kampuni ya Barrick kupitia mgodi wa Bulyanhulu imeendelea kuonesha njia ya kuandaa mustakabali bora wa watoto kwa kuhakikisha wanapata elimu katika mazingira salama na yenye ubora.
Mbali na kuwekeza katika miradi ya kijamii katika vijiji vinavyozunguka mgodi ili kuwawezesha watoto kupata elimu bora na huduma nzuri za kiafya katika maadhimisho ya mwaka huu imewakumbuka wanafunzi wa Msalala na Nyang’hwale wenye matatizo ya kiafya na watokao kwenye kaya zenye mazingira magumu kwa kuwapatia vifaa vya kuwawezesha kusoma katika mazingira rafiki ili waweze kutimiza ndoto zao.
Afisa Mahusiano ya jamii wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo amesema Barrick imekuwa ikiyapa kipaumbele kikubwa masuala yanayohusu watoto ndio maana mwaka huu mgodi umeadhimisha siku yao kwa kutoa msaada wa vifaa vya elimu kwenye watoto wenye changamoto katika Halmashauri za Wilaya za Msalala na Nyang’hwale ikiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali za kuweka mazingira rafiki kwa watoto kuwa na haki sawa na kupata elimu.
Katika shule 15 za Msalala ambazo zimetambulika kuwa na wanafunzi wenye uhitaji wanafunzi wamepatiwa mabegi na madaftari ambapo katika halmashauri ya Nyang’hwale wanafunzi wenye mahitaji kutoka shule 4 zilizopo katika kata ya Mwingiro nao wamenufaika na msaada huo wa vifaa vya kuwasaidia kupata elimu.
"Barrick inayo dhamira ya kuona kila motto katika jamii bila kujali mazingira aliyokulia anapata nafasi ya kusoma,kukua na kutimizia ndoto zake", amesema Senkondo.
Afisa Elimu wa kata ya Bugarama,Bumi Mwasalunjonja ametoa shukrani kwa mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa niaba ya wanufaika wa msaada huu na kwa jinsi mgodi unavyoendelea kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi kijamii inayoendelea kutekelezwa kwa fedha za Uwajibikaji kwa jamii (CSR) ikiwemo kukamilisha ujenzi wa shule ya msingi mpya ya Igudinja ambayo imepunguza adha ya wanafunzi kutembea mwendo mrefu kutafuta elimu.
Naye Mwakilishi wa Afisa Elimu kata ya Mwingiro Juma Asali amesema vifaa vilivyotolewa na Barrick Bulyanhulu kwa kiasi kikubwa vitasaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu kutimiza ndoto zao za kupata elimu sawa na wengine.
Asali amesema miradi ya CSR inayotekelezwa na Barrick Bulyanhulu kwa kushirikiana na Serikali imeleta manufaa kwa wanafunzi na wananchi kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia pamoja na huduma nyingine za kijamii, ikiwemo afya.
Mgodi wa Bulyanhulu unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ikijumuisha sekta za elimu, afya, ujenzi wa barabara na kilimo.
Miradi hiyo pia inalenga kuwawezesha vijana, hususan wanaoishi katika maeneo yanayozunguka mgodi, kupata fursa za kiuchumi na shughuli za kuwaingizia kipato.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464




































