` VIJANA WAPEWA KIPAUMBELE KUIMARISHA MAHUSIANO CHINA NA TANZANIA

WANDAMAN HOTEL

VIJANA WAPEWA KIPAUMBELE KUIMARISHA MAHUSIANO CHINA NA TANZANIA

 


Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam, 12 Agosti 2026

Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mhe. CHEN Mingjian, amesema vijana ndio msingi wa mustakabali wa uhusiano kati ya China na Tanzania. 

Balozi Chen alisema hayo jijini Dar es Salaam leo wakati wa "Mjadala wa China-Tanzania kuhusu Maendeleo na Ubadilishanaji wa Vijana".

Mjadala huo umehudhuriwa na wawakilishi zaidi ya  100 kutoka serikali za China na Tanzania, vyuo vikuu, makampuni ya ujenzi, vyombo vya habari na wanafunzi. Unafanyika katika mwaka maalumu ambapo 2026 inatimiza miaka 70 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Afrika. Pia umetangazwa kuwa "Mwaka wa Ubadilishanaji wa Watu kwa Watu kati ya China na Afrika".

Akifungua mjadala huo, Balozi Chen amesema katika kipindi cha miaka 70 iliyopita, China na Tanzania zimeandika historia nzuri ya udugu na ushirikiano. "Urafiki wetu umepitia vipimo vya muda na umethibitika kwa vitendo. Kuanzia ujenzi wa Reli ya TAZARA hadi Daraja la Nyerere, ushirikiano wetu umeweka watu katikati ya kila kitu," amesema Balozi Chen.

Ameongeza kuwa vijana ni nguvu muhimu katika kujenga "Jumuiya imara kati ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja". Ameeleza matumaini yake matatu kwa vijana. 

Kwanza ni kuwa "wafuatiliaji wa ndoto" wanaounganisha maendeleo yao binafsi na maendeleo ya taifa lao. 

Pili ni kuwa "daraja la kujifunzana" kupitia ubadilishanaji wa utamaduni na heshima kwa pande zote mbili. 

Tatu ni kuwa "nguvu hai" ya maendeleo kwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo ya ufundi stadi, ujenzi, uchumi wa kidijitali na uchumi wa kijani. 

"Urafiki kati ya mataifa yetu unajengwa kwa mawasiliano ya watu kwa watu, na mawasiliano hayo yanategemea vijana. Natumaini ua la urafiki wa China na Tanzania litaendelea kuchanua katika zama hizi mpya," amesema. Pia ametangaza kuwa Ubalozi utashirikiana na wadau kuongeza fursa za masomo ya udhamini na programu za ubadilishanaji wa vijana mwaka ujao.

Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Fredrick Salukele, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Amali Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, amesema urafiki wa Tanzania na China umedumu kwa muda mrefu. Amesema sasa ni wakati wa ushirikiano huo kubadilika kutoka kwenye miundombinu na biashara pekee, na kuelekea kuwaweka vijana, maarifa, ujuzi na uvumbuzi kuwa kitovu cha ushirikiano. 

"Tanzania inatekeleza mageuzi makubwa ya elimu yanayolenga ujuzi, stadi za kidijitali na uhusiano imara na sekta ya viwanda. Ulimwengu wa kazi unabadilika kwa kasi kutokana na Akili Bandia na teknolojia mpya. Mifumo yetu ya elimu inapaswa kubadilika. Tunapaswa kuwaandaa vijana sio tu kwa ajira za leo, bali pia kuwapa uwezo wa kubadilika, ubunifu na stadi za kiteknolojia kwa ajira na biashara za kesho," amesema Dkt. Salukele.

Ametaka kuwepo na ushirikiano zaidi katika elimu ya juu, elimu ya ufundi, mafunzo ya vitendo, na utafiti wa pamoja. Pia amewataka makampuni ya Kichina nchini Tanzania kujumuisha uhamishaji wa ujuzi katika uwekezaji wao. Hii ni pamoja na mafunzo ya ufundi, utafiti, uvumbuzi, uhamishaji wa teknolojia na upatikanaji wa vyeti vya kitaaluma.

"Lengo ni kuunda fursa zaidi za kujifunza kwa vijana wa Kitanzania na kubadilisha 'ubadilishanaji wa watu' kuwa 'ubadilishanaji wa ujuzi'. Pamoja tunaweza kulea kizazi kitakachoweza kuunda mustakabali na kuleta ustawi wa pamoja," amesisitiza. "Daraja imara zaidi kati ya Tanzania na China halitajengwa kwa chuma na saruji tu, bali pia kwa maarifa, ujuzi, urafiki na matarajio ya pamoja ya vijana."

Prof. Baraka J. Maiseli, Mkuu wa Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amezungumzia jukumu la vyuo vikuu katika hatua inayofuata ya ushirikiano. Amekumbuka uzoefu wake kama mwanafunzi wa udhamini wa Serikali ya China kati ya 2012 hadi 2015. "Uzoefu huo ulinipa maarifa mapya, marafiki wa kitaaluma, uzoefu wa utafiti, na kunionyesha nguvu ya elimu ya kimataifa. Nilirejea Tanzania nikiwa na azma ya kuchangia maendeleo ya nchi yetu," amesema Prof. Maiseli.

Alisema kuwa mwaka 2025 pekee, karibu wanafunzi 100 wa Kichina walikuja UDSM kusoma Kiswahili na utamaduni wa Tanzania. 

Pia alitoa wito wa "Mtindo wa Triple-Helix" kwa mustakabali. "Tunahitaji Sekta ya Viwanda kutoa teknolojia, matatizo halisi na ajira. Tunahitaji Vyuo kutoa utafiti, vipaji na uvumbuzi. Na tunahitaji Serikali kubadilisha uvumbuzi kuwa biashara na kuunda mazingira wezeshi. Hawa watatu wakishirikiana, tunaunda ajira na ustawi," amesema. 

Amehitimisha kwa ujumbe kwa vijana: "Vijana wa Kichina na Watanzania wanapaswa kukaa pamoja na kutatua matatizo kwa vitendo. Jengeni ufumbuzi. Anzisheni makampuni. Ongozeni miaka 60 ijayo ya urafiki wa Tanzania na China."

Bw. JIANG YUNTAO, Mwenyekiti wa CRJE (East Africa) na ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Chama cha Makampuni ya Kichina nchini Tanzania, amesema ari iliyoonekana kwa vijana imedhihirisha kuwa mjadala huo ulikuwa na maana. Amesema katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, CRJE imeipa kipaumbele kukuza vipaji vya watanzania. "Kuanzia ujenzi wa Reli ya TAZARA hadi Daraja la Nyerere na miradi mingi zaidi, dhamira yetu imekuwa ile ile: kujenga sio miundombinu tu, bali pia kujenga mauhusiano mwema na watu," amesema Bw. Jiang. 

Amefafanua kuwa kupitia ushirikiano na vyuo na taasisi za ufundi, CRJE imeendelea kutoa fursa kwa vijana wa Kitanzania za kukuza ujuzi, kujifunza kwa vitendo, na ukuaji wa taaluma. Programu hizo ni pamoja na mafunzo kazini, mfumo wa bwana-fundi, mashindano ya ujuzi, na ushirikiano kati ya chuo na kampuni. 

"Tunaamini kuwa ushirikiano endelevu na maendeleo sio tu kuhusu ujenzi wa miradi ya chuma na saruji. Ni pia kusaidia ukuaji wa vijana, kwa sababu wao ndio mustakabali wa taifa," amesema. 

"Mhandisi wa Kichina anapomfundisha kijana wa Kitanzania, na mwanafunzi wa Kitanzania anapoleta maarifa hayo Katika Taifa lake hapo ndipo tunajenga urafiki wa kudumu," amesema.

 Amesisitiza dhamira ya CRJE kuwa ndani ya miaka 10, wahandisi, mafundi na viongozi wa Kitanzania watakuwa wakiongoza miradi mikubwa nchini.

Katika tukio hilo, vijana wa Kitanzania wamesimulia hadithi zao za mafanikio. Mhandisi Titus Lukuwi wa CRJE amesema alianza kama mfanyakazi wa kawaida mwaka 2022. Kupitia mafunzo ya CRJE hatua kwa hatua alijifunza ujuzi wa uhandisi, mawasiliano, utekelezaji wa miradi na viwango vya ubora hadi kuwa miongoni mwa wafanyakazi muhimu wa kiufundi. 

"Nilipopata kazi yangu ya kwanza niliogopa kusema 'sijui'. Lakini CRJE ilitupatia mazingira mazuri. Wahandisi wakubwa walitufundisha kazini," amesema Mhandisi Lukuwi. "Leo niko katika timu inayotengeneza miundombinu ya ubora kwa Tanzania. Matumaini yetu ni kwamba katika miaka michache ijayo wahandisi wa Kitanzania watakuwa na uwezo wa kuongoza miradi kwa ajili ya kampuni na nchi yetu."

Wanafunzi wa UDSM nao wameukaribisha mjadala huo na kusema umewapa matumaini na mwelekeo. Brian Samuel, mwanafunzi wa mwaka wa 3 CoICT, UDSM, akizungumza kwa niaba ya wanafunzi amesema mjadala huo umewaonyesha kuwa ujuzi wao unahitajika kwa maendeleo ya taifa. 

"Tunashukuru UDSM, Serikali ya Tanzania, Ubalozi wa China, na CRJE kwa kuandaa jukwaa hili. Kwa mara ya kwanza tunakaa na Mabalozi, Wahandisi, na Wenyeviti wa Makampuni kuzungumza kuhusu mustakabali wetu," amesema Brian. 

Amesema wanafunzi wengi wa UDSM wanatamani fursa za vitendo. Hatutaki vyeti tu. Tunataka kujenga miradi halisi, kujifunza kutoka kwa wahandisi kazini, na kupata vyeti vinavyohitajika na makampuni," ameongeza. Brian amesema wanafunzi wako tayari kuwa sehemu ya miaka 60 ijayo ya ushirikiano wa Tanzania na China. "Tunaahidi kufanya kazi kwa bidii, kujifunza utamaduni wa Kichina, na kutumia teknolojia kutatua matatizo ya Tanzania katika afya, kilimo na miundombinu.

Wakati wa majadiliano, wahadhiri kutoka vyuo vya China na Tanzania, wafanyakazi wa makampuni ya ndani, wahandisi vijana kutoka miradi ya Kichina, na wataalamu wa rasilimali watu wamejadili changamoto za ushirikiano wa vijana. Wawakilishi wa vijana wamejadili jinsi ya kuoanisha elimu ya ufundi na viwanda vya ndani, kupanua mafunzo ya vitendo kati ya shule na makampuni, na kujenga jukwaa la kudumu la mjadala wa vijana.

Mjadala huu umeandaliwa kwa pamoja na Xufang International Media ya Kundi la Mawasiliano la Kimataifa la China CICG, CRJE, na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464