` SERIKALI YATANGAZA NAFASI ZA UONGOZI TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

WANDAMAN HOTEL

SERIKALI YATANGAZA NAFASI ZA UONGOZI TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

 

Wito umetolewa kwa Watanzania wenye sifa kuomba nafasi za uongozi Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kufuatia kumalizika kwa muda wa kuhudumu wa Makamishna wa sasa kwa mujibu wa Ibara ya 129 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Nafasi ya Mwenyekiti mmoja inahitaji mtu mwenye sifa za kuweza kuteuliwa kuwa Jaji kwa mujibu wa Ibara ya 129 (2) (a) ya Katiba, pamoja na kuwa na uzoefu, maarifa, na ushiriki mpana katika masuala ya sheria, utawala, siasa, na mambo ya kijamii. 

Aidha, mwombaji anapaswa kuwa na uadilifu wa hali ya juu, uwezo mkubwa wa kuandika na kuzungumza Kiswahili na Kiingereza kwa ufasaha, stadi za kutatua migogoro na kushughulikia hali ngumu za kihisia kwa busara, ambapo atalipwa mshahara wa kiwango cha LSSE/8 -1 pamoja na nyongeza ya kuvutia na motisha huku akitekeleza majukumu ya kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu, kupokea malalamiko, kufanya uchunguzi, na kushauri serikali au kufungua mashauri mahakamani kulinda misingi hiyo.

Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti mmoja na Makamishna watano, waombaji wanatakiwa kuwa na ujuzi, uzoefu, na upeo mkubwa katika mambo ya haki za binadamu, sheria, utawala, siasa, au mambo ya jamii kwa mujibu wa Ibara ya 129 (2) (c) ya Katiba, huku wakitakiwa kuwa na sifa za kimaadili yasiyo na dosari, umahiri katika utatuzi wa migogoro, na uwezo wa kufanya kazi kwa ushirikiano au binafsi. 

Makamu Mwenyekiti atapokea mshahara wa kiwango cha LSSE/7 -1 wakati Makamishna watalipwa kiwango cha LSSE/6 -1, ambapo wote kwa pamoja watatekeleza majukumu ya kupokea na kuchunguza malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu, kutoa ushauri kwa umma na taasisi mbalimbali, na kuendeleza usuluhishi miongoni mwa wananchi.

Nafasi za Makamishna Wasaidizi ziko wazi ambapo waombaji wanapaswa kuwa na sifa njema, maadili ya juu, na uadilifu mkubwa kwa mujibu wa kifungu cha 7 (3) cha Sheria ya THBUB Sura ya 391, na watatakiwa kupokea malalamiko kutoka kwa umma, kufanya uchunguzi wa papo hapo, na kutekeleza majukumu mengine watakayopangiwa na tume hiyo kwa kulipwa mshahara wa kiwango cha LSSE4 pamoja na motisha.

Muda na masharti ya kazi kwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, na Makamishna wengine yatazingatia kipindi cha miaka mitatu inayoweza kuteuliwa tena kwa mara moja tu, huku sheria ikimtaka mtu yeyote anayeteuliwa kuacha mara moja nyadhifa zote za kisiasa, ubunge, uongozi wa serikali za mitaa, utumishi wa umma, au uamuzi wa kimahakama ili kuepusha migongano ya kimaslahi.

Barua zote za maombi zinapaswa kuambatana na wasifu wa kina, nakala za vyeti, na barua tatu za mapendekezo kutoka kwa wadhamini, na zitumwe kwa Kamati ya Uteuzi kupitia Mtaa wa Utumishi, Mji wa Serikali Eneo la Mtumba, S. L. P. 1954, Dodoma, au kupitia ofisi zilizopo Shehia ya Mombasa Barabara ya Mkapa Mtaa wa Tawin Zanzibar kwa upande wa visiwani, ndani ya siku 21 tangu kutangazwa kwa nafasi hizo, huku mawasiliano zaidi yakipatikana kupitia namba ya simu 0733122200.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeanzishwa kisheria kupitia Ibara ya 129 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Sura ya Sita, Sehemu ya Kwanza, na kufuatia kumalizika kwa muda wa kuhudumu wa Makamishna wa sasa kwa mujibu wa Ibara ya 129 (4) ya Katiba hiyo, Watanzania wenye sifa sasa wanakaribishwa kuomba kujaza nafasi mbalimbali za uongozi zikiwemo Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Makamishna, na Makamishna Wasaidizi wa tume hiyo ili kusimamia masuala ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464