
Serikali imeeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama nchini kupitia utekelezaji wa maboresho makubwa ya miundombinu, ununuzi wa vitendea kazi vya kisasa na uimarishaji wa mafunzo kwa askari ili kuongeza tija na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kulinda nchi.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, alipokuwa akifanya ziara ya kikazi mkoani Songwe kwa ajili ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali iliyoahidiwa na serikali, ambapo alizindua rasmi mradi wa ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe linalogharimu shilingi bilioni 2.1 pamoja na Kituo cha Zimamoto na Uokoaji katika Wilaya ya Mbozi kilichogharimu shilingi milioni 700.
Waziri Katambi alibainisha kuwa maboresho hayo ya kimkakati yanajumuisha ujenzi na ukarabati wa majengo na ofisi za vyombo vya ulinzi, ununuzi wa magari na vifaa mbalimbali vya utendaji kazi, hatua inayolenga kuhakikisha kuwa askari wanafanya kazi katika mazingira rafiki na yenye tija.
Alifafanua kuwa ziara yake mkoani Songwe inalenga kujionea utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za usalama na maendeleo katika maeneo yao huku taifa likiendelea kuwa ngome ya amani na utulivu kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464