` PROFESA KABUDI AHIMIZA MATUMIZI SAHIHI YA ALAMA ZA TAIFA

WANDAMAN HOTEL

PROFESA KABUDI AHIMIZA MATUMIZI SAHIHI YA ALAMA ZA TAIFA

  

Na Mwandishi wetu- DODOMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, amehimiza wananchi kuendelea kuzingatia matumizi sahihi ya alama za Taifa, hususan rangi na mwonekano wa Bendera ya Taifa, kwa mujibu wa sheria.

Prof. Kabudi ametoa kauli hiyo leo, Agosti 12, 2026, jijini Dodoma, alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala wa Serikali wa Uchapishaji Tanzania, ambapo alipongeza taasisi hiyo kwa kuendelea kuelimisha umma na kusimamia matumizi sahihi ya alama za Taifa, ikiwemo Bendera na Nembo ya Taifa.

Amesema sheria inayosimamia matumizi ya alama za Taifa inaweka wajibu kwa Wakala wa Serikali wa Uchapishaji Tanzania kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa ipasavyo, ikiwemo kuzalisha Bendera za Taifa kwa niaba ya Serikali.

“Sheria ya Alama za Taifa inaeleza kuwa Bendera yetu ina ufito wa rangi ya dhahabu na siyo njano. Lazima tuzingatie sheria ilivyoelekeza na kuendelea kuelimisha umma kuhusu matumizi na rangi sahihi za Bendera ya Taifa,” amesisitiza Prof. Kabudi.

Aidha, Prof. Kabudi amesema mabadiliko ya Idara kuwa Wakala wa Serikali yanalenga kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali, pamoja na kuiwezesha taasisi hiyo kuendelea kupanua shughuli zake kulingana na mabadiliko ya teknolojia, uchumi na mahitaji ya kimkakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wakala wa Serikali wa Uchapishaji Tanzania, Bw. George Lugome, amesema Wakala unaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa mashine mpya na malighafi, kulingana na mahitaji ya uzalishaji.

Amesema uwekezaji huo unalenga kuimarisha uwezo wa Wakala katika uzalishaji na utoaji wa huduma kwa ufanisi, sambamba na kuendana na mahitaji ya sasa ya kiteknolojia.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464