` MBUNGE AZZA AENDELEA KUCHANJA MBUGA, KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI WA JIMBO LA ITWANGI KIJIJI KWA KIJIJI

WANDAMAN HOTEL

MBUNGE AZZA AENDELEA KUCHANJA MBUGA, KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI WA JIMBO LA ITWANGI KIJIJI KWA KIJIJI

 


Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Masunula kata ya Usule, Agosti 15, 2026.


TAZAMA VIDEO👇👇


Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Masunula kata ya Usule, Agosti 15, 2026.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwamala, Kata ya Mwamala, Agosti 15, 2026.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwamala, Kata ya Mwamala, Agosti 15, 2026. Picha na Kadama Malunde

Na Marco Maduhu – SHINYANGA

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, ameendelea kuchanja mbuga kwa kufanya ziara ya kijiji kwa kijiji katika jimbo hilo, akilenga kusikiliza kero za wananchi na kuzitolea majibu pamoja na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Leo, Agosti 15, 2026, Mbunge huyo ametembelea Vijiji vya Masunula kata ya Usule na Mwamala kata ya Mwamala, ambapo wananchi wamejitokeza kwa wingi na kuwasilisha changamoto mbalimbali, zikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa huduma ya maji na umeme katika baadhi ya vitongoji pamoja na ukosefu wa zahanati katika Kijiji cha Masunula.

Akizungumza na wananchi katika mikutano hiyo, Azza amesema changamoto hizo tayari amezifanyia kazi na kuzifikisha Bungeni, huku baadhi zikiwa zimeanza kupata ufumbuzi na nyingine zikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Akizungumzia suala la umeme, amesema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030 inaelekeza kuwa ifikapo mwaka huo vitongoji vyote nchini viwe vimefikiwa na huduma ya umeme.
Amesema katika utekelezaji wa azma hiyo, Jimbo la Itwangi limefanikiwa kupata umeme katika vitongoji 58, huku akiwataka wananchi ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo kuwa na subira.

“Niwatoe hofu wananchi katika vitongoji ambavyo bado havijapata umeme; wote watapata huduma hii kwa sababu maendeleo ni hatua kwa hatua,” amesema Azza.

Akizungumzia barabara ya Masunula–Usanda, Azza amesema tayari fedha zimepatikana kwa ajili ya ujenzi wa daraja lililokuwa changamoto kubwa kwa wananchi, hasa wakati wa msimu wa mvua, na kwamba mchakato wa utekelezaji umeanza baada ya kazi hiyo kutangazwa.

Pia amezungumzia barabara ya Masunula–Tinde Mnadani, akisema kwa muda mrefu ilikuwa katika hali mbaya na haikupitika wakati wa msimu wa mvua.
Amesema baada ya wananchi kuwasilisha changamoto hiyo, aliendelea kuisemea hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, aliposikia kilio cha wananchi na kutoa Shilingi milioni 300 kwa ajili ya uboreshaji wa barabara hiyo.

Amesema fedha hizo zimetumika katika ujenzi wa barabara pamoja na daraja, hivyo kwa sasa barabara hiyo inapitika.

Katika suala la maji, Azza amesema changamoto ya upatikanaji wa maji ni miongoni mwa ajenda kubwa katika Jimbo la Itwangi, akieleza kuwa amekuwa akiwasilisha suala hilo Bungeni na kufanya mazungumzo na Wizara ya Maji.

Amesema kupitia juhudi hizo, amefanikiwa kupata mtambo wa kuanza kuchimba visima vya maji wakati Serikali ikiendelea na mipango ya kupeleka maji kutoka Ziwa Victoria katika maeneo husika.

Azza pia amezungumzia changamoto ya uchakavu wa miundombinu katika Shule ya Msingi Masunula, pamoja na ukosefu wa choo cha walimu, akisema tayari ameanza kuzifanyia kazi changamoto hizo.

Akizungumza na wananchi wa Mwamala, amesema changamoto kubwa inayowakabili ni upatikanaji wa maji.
Amesema kuna mradi wa maji unaotekelezwa katika eneo hilo ambao umesimama kwa muda mrefu, hivyo ameliwasilisha suala hilo Bungeni ili hatua zaidi zichukuliwe na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo.

Ziara hiyo ya Mbunge Azza ni sehemu ya mpango wake wa kutembelea vijiji mbalimbali ndani ya Jimbo la Itwangi, kusikiliza changamoto za wananchi moja kwa moja na kufuatilia utekelezaji wa ahadi pamoja na miradi ya maendeleo.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464