` UMUHIMU WA CHAKULA KWA WANAFUNZI SHULENI WASISITIZWA KUONGEZA UFAULU, KIKAO CHA BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI (W) SHINYANGA

WANDAMAN HOTEL

UMUHIMU WA CHAKULA KWA WANAFUNZI SHULENI WASISITIZWA KUONGEZA UFAULU, KIKAO CHA BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI (W) SHINYANGA

 



Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga Said Kitinga, amesisitiza umuhimu wa wanafunzi kupata chakula wakiwa shuleni, ili kuongeza ufaulu katika masomo yao na kuondokana na kero ya kusoma wakiwa na njaa.

Kitinga amebainisha hayo leo, Agosti 13, 2026, wakati akitoa salamu za wilaya, kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya hiyo.
Amesema, madiwani pamoja na watendaji wanapaswa kushirikiana kwa karibu na kamati za shule pamoja na wazazi kupitia vikao vya pamoja, ili kuhakikisha huduma ya chakula inapatikana kwa wanafunzi wote shuleni.

“Zipo tafiti zinazothibitisha kuwa shule, nyingi zinazofanya vizuri kitaaluma zinachangiwa na wanafunzi kupata chakula wakiwa shuleni,” amesema Kitinga.
Katika hatua nyingine, ameipongeza shule ya sekondari ya wasichana ya Tinde, kutokana na kuonyesha ufanisi mkubwa kitaaluma na kupata ufaulu wa juu katika matokeo ya kidato cha sita.

Naye Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad, amekazia suala hilo la lishe mashuleni, huku akiipongeza kata ya Didia wilayani humo kwa kuhakikisha shule zote zinatoa huduma ya chakula kwa wanafunzi.
Amesisitiza kuwa suala hilo la chakula, linapaswa kusimamiwa kikamilifu kupitia vikao vya mara kwa mara na wazazi, ili kuondoa changamoto ya watoto kusoma wakiwa na njaa.

Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk. Kalekwa Kasanga, akiwasilisha taarifa yake kwenye baraza hilo, amesema katika sekta ya elimu, shule ya Sekondari ya wasichana Tinde, imepata ufaulu wa asilimia 100 katika matokeo ya kidato cha sita.

Dk. Kasanga ameeleza kuwa, kati ya watahiniwa 347 waliofanya mtihani huo, wanafunzi 101 wamepata daraja la kwanza, 201 wamepata daraja la pili, huku 45 wakipata daraja la tatu.
Amesema, mafanikio hayo makubwa yamechangiwa na ushirikiano mzuri uliopo kati ya wazazi, walimu na wadau wa elimu katika kufuatilia maendeleo ya wanafunzi.

Aidha, katika baraza hilo yalizungumza mambo mbalimbali likiwamo suala ya ukusanyaji wa mapato, huduma za umeme, maji pamoja na barabara, huku wananchi wakisisitiwa pia kutunza vyakula, pamoja na kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye Mwenge wa uhuru wilayani humo, utakaokimbizwa kuanzia Agosti 20 hadi 21 na kisha kukabidhiwa wilayani Kahama, ambapo kimkoa utapokelewa Agosti 18 ukitokea mkoa wa Mwanza.


TAZAMA PICHA👇👇
Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga Said Kitinga akizungumza.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Seth Msangwa akizungumza.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk.Kalekwa Kasanga akiwasilisha taarifa yake..
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464