Bandora ametoa wito huo wakati akiendelea kutembelea maeneo mbalimbali katika kata za Manispaa ya Tabora, ambako amekuwa akitoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira na namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika kuyatunza.
Amesema usafi wa mazingira haupaswi kuonekana kuwa ni jukumu la viongozi pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi na unapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku.
Amesisitiza wananchi kuhakikisha maeneo yao ya makazi, biashara na maeneo ya umma yanakuwa safi kwa kufanya usafi mara kwa mara, pamoja na kutupa taka katika maeneo maalumu yaliyotengwa na serikali za mitaa.
“Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha mazingira yanayomzunguka yanakuwa safi. Tusisubiri kuamriwa au kushurutishwa na viongozi ndipo tufanye usafi,” amesema Bandora.
Aidha, Bandora ameahidi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kusimamia utekelezaji wa shughuli za usafi katika maeneo mbalimbali, akilenga kuona Manispaa ya Tabora inakuwa safi, salama na yenye mazingira bora kwa wananchi.
Amesema usafi wa mazingira ni jukumu la kisheria na kijamii linalolenga kulinda afya za wananchi, kupunguza hatari ya magonjwa ya mlipuko na kuhakikisha mazingira ya makazi na biashara yanatunzwa ipasavyo.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa wananchi, viongozi na wadau mbalimbali ni muhimu katika kufanikisha azma ya kuwa na mazingira safi na salama katika Manispaa ya Tabora.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464



