
Serikali imewapongeza wananchi wa Tanzania kwa kuamua kupuuza na kukataa mwito uliokuwa umetangazwa wa kutaka kuvuruga amani ya nchi hivi karibuni mnamo Julai Saba.
Pongezi hizo zimetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipotembelea maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, ambapo alibainisha kuwa kuna kikundi cha watu waliopo ndani na nje ya nchi wanaojificha na kujaribu kuelekeza Watanzania kwenye njia itakayoangamiza uchumi. Msigwa alisisitiza kuwa taifa haliwezi kufikia malengo makubwa ya maendeleo endapo wananchi wataendelea kupoteza muda wao wa uzalishaji kwenye migogoro, malalamiko na vitendo vinavyovuruga amani, na badala yake akahimiza kudumishwa kwa utulivu ili nchi ibaki kuwa kisiwa cha amani na mazingira rafiki kwa uwekezaji.
Msemaji Mkuu huyo alionya kuwa watu wanaohamasisha vurugu hizo wakiwa mataifa ya nje wenyewe wanafanya kazi kwa bidii huku nchi wanazoishi zikiwa tulivu, hivyo akawataka Watanzania kuangalia ukweli huo na wasikubali kushinda barabarani bila kulima, kufanya biashara au kuchimba madini kwa kuwa kufanya hivyo ni kujiharibia wenyewe.
Alibainisha kuwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kukuza wastani wa kipato cha Mtanzania kutoka Sh milioni 3.5 hadi kufikia Sh milioni 18 kwa mwaka yatafikiwa tu iwapo kila mmoja ataongeza bidii na kufanya kazi mara tatu zaidi ya sasa.
Msigwa alisema ongezeko la uzalishaji ndilo litakalosaidia kupunguza umaskini, kuongeza kipato na kuboresha huduma za kijamii ikiwemo sekta ya afya nchini.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464