
Kampeni ya "Mjue Jirani Yako" imepewa msukumo mpya mkoani Tabora baada ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala, kuwataka Maafisa na Askari wa Uhamiaji kuifikisha kwa wananchi kwa nguvu zaidi ili kuimarisha mapambano dhidi ya uhamiaji haramu na kuendelea kulinda amani na usalama wa Taifa.
Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi mkoani humo, Dkt. Makakala amesisitiza kuwa mafanikio ya kampeni hiyo yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama kupitia utoaji wa taarifa sahihi kuhusu wageni wasiowafahamu katika maeneo yao.
Mbali na kusisitiza utekelezaji wa kampeni hiyo, Dkt. Makakala amewataka Maafisa, Askari na Watumishi wa Umma kuongeza weledi, uwajibikaji na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ili Idara iendelee kutoa huduma bora zinazokidhi matarajio ya wananchi.
Aidha, ameeleza kuwa mafanikio yanayoendelea kupatikana ndani ya Idara ya Uhamiaji yanatokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan.