Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, kwa kufanikiwa kupata Hati Safi mara tano mfululizo katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
TAZAMA VIDEO👇👇
Mhita ametoa pongezi hizo leo Julai 9, 2026, wakati akitoa salamu za mkoa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Manispaa ya Shinyanga, kilichokuwa na ajenda ya kupokea na kujadili hoja za CAG kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Amesema kuwa anaipongeza halmashauri hiyo kwa kazi nzuri inayofanya na kuacha rekodi hiyo safi, huku akitoa maelekezo kwa watendaji kuhakikisha hoja zote zilizosalia zikiwamo za miaka ya nyuma, zinajibiwa mapema na kufungwa.
"Nawapongeza sana Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa kupata Hati Safi mara tano mfululizo, hongereni sana kwa kazi nzuri," amesema Mhita.
Mbali na mafanikio hayo ya kifedha, Mkuu huyo wa mkoa ameipongeza pia manispaa hiyo kwa kuwa kinara nchini Tanzania kwa kuongoza katika suala la usafi wa mazingira.
Katika hatua nyingine, Mhita ameagiza uongozi wa halmashauri hiyo kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani, ili kuendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, pamoja na kuwapatia fursa za zabuni kwenye miradi mbalimbali inayotekelezwa na halmashauri.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Arnold Makombe, ameungana na Mkuu wa Mkoa kuipongeza manispaa hiyo kwa kuendelea kupata Hati Safi na kusimamia vizuri fedha za umma.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo, amesema maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa yatafanyiwa kazi kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kufunga hoja zote za CAG zilizopo kwenye hatua ya utekelezaji. na kuongeza nguvu kwenye ukusanyaji wa mapato.
Awali, Mweka Hazina wa Manispaa ya Shinyanga CPA Mulokozi Kishenyi, akiwasilisha taarifa hiyo ya CAG, amethibitisha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 manispaa hiyo imepata Hati Safi.
Kishenyi amebainisha kuwa katika mwaka huo wa fedha walikuwa na jumla ya hoja 21, ambapo hoja nne tayari zimefungwa, na hoja 17 zilizosalia zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza huku akionyesha furaha kwa Manispaa ya Shinyanga kupata hafi safi mara tano mfululizo.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Anold Makombe akizungumza.
Katibu tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni akiwa kwenye kikao cha madiwani cha kujadili hoja za CAG.