` KISHAPU YANG’ARA KWA KUPATA HATI SAFI MARA TANO MFULULIZO, MKURUGENZI AMWAGIWA SIFA KILA KONA

WANDAMAN HOTEL

KISHAPU YANG’ARA KWA KUPATA HATI SAFI MARA TANO MFULULIZO, MKURUGENZI AMWAGIWA SIFA KILA KONA

 

Na Marco Maduhu, KISHAPU

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kufanikiwa kupata hati safi mara tano mfululizo, katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akibainisha kuwa mafanikio hayo yanaonyesha uadilifu na uzalendo mkubwa katika matumizi ya fedha za umma.

TAZAMA VIDEO👇👇


Ametoa pongezi hizo leo Julai 10, 2026, wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, kilichokuwa na ajenda ya kupokea na kujadili hoja za CAG kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo halmashauri hiyo imeendeleza wimbi lake la ushindi wa hati hizo safi.
Amempongeza Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mkurugenzi na wataalamu wote, kwa kuendelea kupata hati safi kwa vipindi vitano mfululizo, na kuonyesha uadilifu, uzalendo katika matumizi ya fedha za maendeleo ambazo zinaletwa kwa mustakabali wa wananchi.

“Upatikanaji wa hati hii safi, waheshimiwa madiwani wana nafasi kubwa sana, sababu baraza lenye umoja na mshikamano, kati ya timu ya madiwani na menejimenti siku zote huwezi kukutana na changamoto,” amesema Mhita.
“Nitumie pia fursa kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, waheshimiwa madiwani niwaambie tu kwamba kwakweli kama Mkurugenzi mmepata, mna Mkurugenzi kweli kweli, ambaye anadhamira ya dhati ya kulinda maslahi, Rasilimali na fedha za maendeleo ambazo mheshiwa Rais anazileta kwenye halmashauri kwa maslahi ya wananchi,” ameongeza Mhita.

Pamoja na pongezi hizo, Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza viongozi na wataalamu wa halmashauri zote mkoani humo, kuhakikisha wanakuwa na usimamizi madhubuti wa fedha za miradi ya maendeleo, huku akisisitiza kuwa thamani halisi ya fedha hizo lazima ionekane kupitia ubora wa miradi inayotekelezwa.
Amesema kuwa hakupaswi kuwe na kigugumizi chochote katika kulinda rasilimali za umma na kusimamia fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambazo zinatolewa na serikali kwa ajili ya maslahi na mustakabali mpana wa wananchi.

“Binafsi sina kigugumizi na sijawahi kuwa na undumilakuwili linapokuja suala la kusimama imara, kutetea, na kupigania fedha ambazo kiongozi wetu mkuu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, anazileta kwenye maeneo yetu ili ziwafikie wananchi. Popote penye kona kona tutasimama imara,” amesema Mhita.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kishapu Peter Masindi, ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi mara tano mfululizo.

Awali akiwasilisha taarifa hiyo ya ukaguzi wa CAG kwa mwaka huo wa fedha, Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu George Silumbwe, alisema walikuwa na jumla ya hoja 32, ambapo hoja tano zimefungwa, huku hoja 27 zilizobaki zikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji, hali iliyowezesha halmashauri hiyo kuibuka na hati safi.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Josephat Limbe, alishukuru kwa pongezi hizo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na kueleza kuwa maelekezo yote yaliyotolewa watayazingatia na kuyatekeleza kikamilifu ili kuendeleza ufanisi na nidhamu hiyo ya fedha.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Peter Masindi akizungumza.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Emmanuel Johnson akizungumza.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Emmanuel Johnson akizungumza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Josephat Limbe akizungumza.
Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu George Silumbwe akiwasilisha taarifa ya CAG.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464