MANISPAA SHINYANGA YAPANDA MITI 985,000 KWA MWAKA MMOJA
Na Mwandishi Wetu , SHINYANGA
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imefanikiwa kupanda miti 985,000 katika shule, vituo vya afya, maeneo ya wazi na kando ya barabara katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Hayo yameelezwa leo Juni 5, 2026 na Afisa Mazingira wa Manispaa ya Shinyanga, Gidai, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira.
Amesema pamoja na mafanikio hayo, wananchi zaidi ya 15,000 wamepatiwa elimu kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa kutunza mazingira, huku kaya 800 zikihamasishwa kutumia majiko banifu na nishati safi badala ya kuni.
Maadhimisho hayo yameshirikisha wanafunzi wa Chuo cha Serikali za Mitaa, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Joseph Muhunda Nyerere Foundation na wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Miti Mirefu, Nassor Mokhe Waryioba, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amewataka wananchi kuendelea kupanda na kutunza miti ili kuboresha mazingira, kuongeza usafi wa mji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, ameipongeza TFS kwa juhudi zake za kuendeleza shughuli za uhifadhi wa misitu na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Joseph Muhunda Nyerere Foundation, Chief Muhunda Nyerere, amesema taasisi hiyo imefanikiwa kupanda miti zaidi ya 9,000 katika Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu.
Naye Muhifadhi wa Misitu kutoka TFS, Franaeli Sumari, amewahimiza wananchi kuendelea kutunza mazingira na kuhifadhi rasilimali za taifa, huku akibainisha kuwa taasisi hiyo inaendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa misitu pamoja na kugawa miche ya miti kwa wananchi.
Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa viongozi, wadau wa mazingira na wananchi kushiriki zoezi la upandaji miti katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu ya mwaka huu inayosema, "Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050: Tuwajibike kukijanisha Tanzania."























