` GHARAMA ZA UENDESHAJI ZATAJWA MABADILIKO BEI MPYA ZA MAJI SHUWASA

WANDAMAN HOTEL

GHARAMA ZA UENDESHAJI ZATAJWA MABADILIKO BEI MPYA ZA MAJI SHUWASA



Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Mamlaka ya Majisafi na usafi wa mazingira Shinyanga (SHUWASA) imetaja sababu ya mabadiliko bei mpya za maji, kuwa inatokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi yaliyosababisha kupanda kwa gharama za uendeshaji wa utoaji wa huduma za maji.

TAZAMA VIDEO👇👇
Mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Yusup Katopola, ametaja miongoni mwa sababu zilizochangia marekebisho hayo ya bei mpya za maji kuwa ni kuongezeka kwa gharama za ununuzi wa maji ya jumla, dawa za kutibu maji, pamoja na gharama za ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya maji kupanda.

Amebainisha hayo leo Juni 6,2026 kwenye kikao cha wadau wa huduma za maji manispaa ya Shinyanga, cha kujadili na kupitisha mabadiliko ya bei mpya za maji kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma hiyo.
“Tumefanya marekebisho haya kutokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji wa huduma za maji. Lengo letu ni kuhakikisha huduma inaendelea kutolewa kwa ufanisi na ubora unaostahili kwa wananchi,” amesema Katopola.

Kaimu Mkurugenzi wa huduma kwa wateja wa SHUWASA, Reuben Mwandumbya ametaja viwango vipya vya bei za maji vitakavyoanza kutumika katika mwaka wa fedha 2026/27, kuwa wateja wa majumbani wanaotumia zaidi ya mita za ujazo tano kwa mwezi watalipa Sh. 1,840 kwa mita ya ujazo kutoka Sh. 1,740 za sasa.
Taasisi mbalimbali zitalipa Sh. 3,060 kwa mita ya ujazo kutoka Sh. 2,760, huku wateja wa sekta ya biashara wakiongezeka kutoka Sh. 2,790 hadi Sh. 3,100 kwa mita ya ujazo",ameeleza Mwandumbya.

Aidha, amebainisha kuwa, gharama za huduma ya maji kwa viwanda zimeongezeka kutoka Sh. 2,850 hadi Sh. 3,160 kwa mita ya ujazo, wakati viwanda vya vinywaji vitatozwa Sh. 4,160 kutoka Sh. 3,750 za awali. Kwa upande wa vibanda vya kuuza maji, kiwango kipya kitakuwa Sh. 1,670 kwa mita ya ujazo kutoka Sh. 1,500 zilizokuwa zinatumika hapo awali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, amesema SHUWASA iliwasilisha ombi la marekebisho ya bei hizo za maji kwa Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (EWURA) tangu mwaka 2022, lakini mchakato huo umekamilika mwaka 2026 na kutangazwa rasmi kupitia Gazeti la Serikali.

Amesema, baada ya kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali, viwango hivyo vipya vinakuwa na nguvu ya kisheria na vitaanza kutumika rasmi kuanzia Julai 1, 2026, na kusisitiza wananchi wapatiwe elimu ya kutosha juu ya mabadiliko ya bei hizo mpya za maji.
Nao baadhi ya wadau hao wa maji wakiwamo wawakilishi wananchi, wamesisitiza elimu itolewe zaidi kwa wananchi, ili waelewe mabadiliko hayo ya bei mpya za maji itakayo saidia kupuguza kero na malalamiko ya bei hizo.

MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA Ruben Kitinya akizungumza.
Mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza.
Kaimu Mkurugenzi wa huduma kwa wateja wa SHUWASA, Reuben Mwandumbya akiwasilisha taarifa ya bei mpya za maji.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464