Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius mtatiro akizungumza kwenye baraza la madiwani
Na Suzy Butondo, Shinyangapressblog
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amewataka madiwani wa Manispaa ya Shinyanga kuhakikisha wenyeviti wa mitaa wanachukua hatua kali dhidi ya kampuni za mikopo zinazowavamia wananchi na kuwachukulia mali zao kwa nguvu.
Akizungumza leo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga, Mtatiro amesema baadhi ya kampuni za mikopo zimekuwa zikitoa mikopo kwa wananchi lakini baadaye kuwafuata mitaani na hata kuvamia makazi yao pindi wanapochelewa kurejesha fedha hizo.
Amesema tayari serikali ya wilaya imekubaliana kuwa ni marufuku kwa kampuni hizo kwenda kwenye maeneo ya wananchi kwa lengo la kuwasumbua au kuwanyang’anya vifaa vyao vya kazi.
“Ni kweli makampuni haya yapo kisheria na yana leseni pamoja na ofisi rasmi, lakini si sahihi kuvamia wananchi na kuwachukulia vifaa vinavyowasaidia kujipatia kipato.
"Wengine hata mikataba yao bado haijaisha lakini tayari wananyang’anywa mali zao, hili halikubaliki,” alisema Mtatiro.
Aidha, amewataka madiwani na viongozi wa mitaa kuhakikisha kampuni zitakazobainika kufanya vitendo hivyo zinakamatwa mara moja.
Katika hatua nyingine, Mtatiro amewataka wataalamu wa halmashauri kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kufikia lengo la asilimia 100, akibainisha kuwa kwa sasa ukusanyaji umefikia asilimia 60 pekee.
“Nimuombe mkurugenzi aje na mkakati wa wazi wa namna ya kuongeza ukusanyaji wa mapato katika kipindi hiki kilichobaki, kwani bado tuna asilimia 40 kufikia lengo, hivyo ni muhimu kuongeza kasi,” amesema.
Akizungumzia changamoto ya watoto wa mitaani, amewataka madiwani kushirikiana katika kuwasaidia watoto hao ambao wengi wao wanaishi mazingira magumu na kukosa mahitaji muhimu.
Amesema baadhi ya watoto hao wamekuwa wakitamani kupata nafasi za kujiunga na vyuo vya ufundi stadi ili wajifunze ujuzi utakaowasaidia kujitegemea na kuachana na maisha ya mitaani.
“Hili ni tatizo letu sote. Shinyanga inajulikana kwa watu wachapakazi na watoto wengi wa mitaani wanatoka hapa hapa wilayani, hivyo lazima tushirikiane kuwasaidia,” amesema.
Kwa upande wao, madiwani wa Manispaa ya Shinyanga wamelalamikia ubovu wa barabara katika maeneo yao na kuiomba TARURA kuzifanyia matengenezo ili kurahisisha usafiri kwa wananchi.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Salum Kitumbo amewataka madiwani kudumisha umoja na ushirikiano ili kuifikisha manispaa hiyo kwenye hadhi ya jiji, akisisitiza kuwa maendeleo ya manispaa yanahitaji mchango wa kila mmoja.