` SHINYANGA KUTOA CHANJO YA POLIO AWAMU YA PILI

WANDAMAN HOTEL

SHINYANGA KUTOA CHANJO YA POLIO AWAMU YA PILI


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ,Mboni Mhita akizungumza kuhusu utoaji wa chanjo ya polio awamu ya pili.


Na Mwandishi Wetu

Serikali ya Mkoa wa Shinyanga imejizatiti kutoa chanjo ya matone ya polio kwa awamu ya pili kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 10, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha afya ya watoto katika mkoa huo.

Akizungumza na vyombo vya habari leo, Mei 6, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, alisema kuwa zoezi hilo litafanyika kuanzia Mei 7 hadi Mei 10, likilenga kuwafikia watoto wote walio chini ya umri huo ili kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa polio.

“Uwekezaji katika afya ya watoto ni muhimu kwa ustawi wao. Watoto wanapokuwa na afya njema, huwapa wazazi na walezi nafasi ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi,” alisema Mhita.

Aidha, Mhita alisisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa afya watakaopita kwenye kaya, vituo vya afya, pamoja na maeneo yenye mikusanyiko ya watu, ili kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo hiyo.

“Ni muhimu kuepuka taarifa potofu na upotoshaji unaoweza kukwamisha zoezi hili muhimu la afya ya jamii,” aliongeza.

Katika awamu ya kwanza ya chanjo hiyo, zaidi ya watoto laki tisa walifanikiwa kufikiwa kupitia timu za wataalamu wa afya waliotembelea kata zote 130 za Mkoa wa Shinyanga.

Kwa upande wake, Mratibu wa Chanjo Manispaa ya Shinyanga, Moses Mwita, alisema kuwa katika awamu hii wamewahusisha watu wenye ushawishi katika jamii ili kusaidia utoaji wa elimu kwa wananchi. Pia wataalamu wa afya wamepewa mbinu wezeshi za kuhakikisha huduma bora inatolewa kwa wananchi.

Sekta ya afya imeendelea kupata maboresho makubwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, ununuzi wa vifaa tiba, ujenzi wa nyumba za watumishi, utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, pamoja na ajira za watumishi wa afya na ongezeko la madaktari bingwa.

Mratibu wa chanjo-manispaa ya Shinyanga,Moses Mwita



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464