` RC DAR AONYA UKUMBATIAJI WA PROPAGANDA ZA CHUKI

WANDAMAN HOTEL

RC DAR AONYA UKUMBATIAJI WA PROPAGANDA ZA CHUKI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka vijana kuachana kabisa na propaganda za chuki na badala yake waelekeze akili na nguvu zao katika juhudi za kujiletea maendeleo. 

Chalamila alisema kuwa maisha ya sasa yanahitaji uvumilivu, juhudi, na kujituma kwa kasi kubwa, kwani mafanikio ya kweli hayaji kwa kupiga maneno mengi au kueneza chuki mitandaoni. 

Alionya kuwa siasa za majitaka zinaweza kuharibu mustakabali wa maisha yao na kuongeza kuwa, licha ya elimu wanayoipata, mtihani mkubwa na wa kweli upo katika uwezo wao wa kujimudu kimaisha na namna wanavyoyatafsiri maisha kwa vitendo.

Chalamila alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati wa kongamano la wanafunzi wa vyuo vikuu lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) lililojadili nafasi ya vijana katika kulinda amani, mshikamano, na maendeleo ya taifa.

Kwa upande wa ngazi ya wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, alitangaza mkakati kabambe unaolenga kuwainua vijana kwa kuanza mpango wa kuwarasimisha zaidi ya waendesha bodaboda 9,000 ili kuwawezesha kupata vyeti vya kuzaliwa, leseni, namba za mlipakodi (TIN), pamoja na mikopo yenye masharti nafuu. 

Mpango huo unaotekelezwa katika mitaa yote 90 ya Wilaya ya Ubungo una lengo la kuwasaidia vijana kujitegemea na kuwatoa kwenye utumwa wa mikataba ya kinyonyaji ya ukodishwaji wa vyombo vya moto, ili hatimaye waweze kujikomboa kiuchumi kwa kutumia fursa zilizopo ndani ya maeneo yao.

Naye aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Victoria, Ezekiah Wenje, alitoa angalizo kuhusu baadhi ya wanasiasa wanaotumia mitandao ya kijamii kuwapotosha vijana kwa ajili ya kujitafutia umaarufu binafsi. 

Wenje,  alilinganisha kitendo cha kumpa nchi mwanasiasa wa namna hiyo na kumpa mtoto msumeno, kwani atakata kila kitu bila kujua madhara yake. 

Aliwataka vijana kutambua wajibu wao mkuu wa kulinda taifa lao bila kujali tofauti zao za kiitikadi, akifafanua kuwa serikali huja na kuondoka kama zinavyobadilika vyama nchini Marekani, lakini msingi mkubwa na wa kudumu wakati wote lazima ubaki kuwa ni taifa lenyewe.

  

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464