Mtandao wa Wamiliki wa Nyumba za Upataji Nafuu nchini, Tanzania Network for Voice of Sober House Tanzania, umemkabidhi tuzo ya shukrani Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, kwa kutambua mchango wake mkubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya hususan katika eneo la usimamizi, uratibu na uwezeshaji wa nyumba za upataji nafuu nchini.
Tuzo hiyo ilitolewa ikiwa ni ishara ya kuthamini ushirikiano na mchango wa DCEA katika kuimarisha huduma za uokoaji, uangalizi na urejeshwaji wa waathirika wa dawa za kulevya kupitia nyumba za upataji nafuu zinazofanya kazi kwa kushirikiana na Mamlaka.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwenyekiti wa mtandao huo, Khamis Swuwira, amesema kuwa wamekuwa wakipata ushirikiano mkubwa kutoka DCEA kila wanapohitaji msaada, miongozo na ushauri wa kitaalamu katika utekelezaji wa majukumu yao.
“DCEA imekuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha nyumba za upataji nafuu zinafanya kazi kwa kuzingatia taratibu, weledi na malengo ya kuwasaidia waathirika kurejea katika maisha yenye tija,” amesema Swuwira.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa mtandao huo, Saidi Bandawe, amesema Kamishna Jenerali pamoja na DCEA kwa ujumla wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa vitendo, hali ambayo imeendelea kuleta matumaini kwa waathirika na jamii kwa ujumla.
Naye Mjumbe wa Bodi ya mtandao huo, Pilli Misana, amepongeza juhudi za DCEA katika kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa huduma za urejeshwaji na uangalizi wa waraibu wa dawa za kulevya nchini.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo ameushukuru mtandao huo kwa kutambua mchango wa DCEA na kusisitiza kuwa Mamlaka itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na kusaidia mifumo ya urejeshwaji wa waathirika ili kujenga jamii salama na yenye nguvu kazi yenye afya.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464













