
Serikali imepata mafaniko makubwa katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2020/2021 hadi 2025/2026 kwa kuwezesha sekta ya kilimo kuwa ya kisasa zaidi nchini.
Hatua hii inakuja wakati muafaka ambapo taifa linakumbushwa ripoti na sababu zilizotolewa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman kuhusu vurugu zilizotokea nchini tarehe 29 Oktoba, ambapo alibainisha wazi kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ndiyo uliokuwa kichocheo kikubwa cha machafuko hayo ya kijamii.
Sekta hii ya kilimo inayochangia asilimia 27 ya Pato la Taifa na asilimia 24 ya mauzo ya nje, inatajwa kama sekta mkombozi inayoweza kufuta kabisa tatizo la ukosefu wa ajira na kuleta amani ya kudumu nchini.
Ili kukabiliana na ukosefu huo wa ajira na kuzuia viashiria vya uvunjifu wa amani, serikali imeweka nguvu kubwa katika matumizi ya teknolojia na tafiti ili kuongeza tija na kuvutia vijana wengi zaidi kwenye sekta hii.
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, ameliambia Bunge kuwa hadi sasa wizara imeanzisha vituo 79 vya kutoa huduma za zana za kisasa ambapo matrekta 360 yameshasambazwa, huku kukiwa na mpango kabambe wa kununua matrekta makubwa na madogo 10,000 pamoja na mashine za kuvunia. Mabadiliko haya ya kutoka kwenye kilimo cha jembe la mkono kwenda kilimo cha mitambo yanalenga kubadilisha mtazamo wa vijana ili waone kilimo kama biashara yenye faida itakayowapatia ajira za uhakika.
Mbali na zana hizo, serikali imeanzisha mfumo wa kidijiti wa e-Kilimo ambao unawawezesha vijana wasomi kupata ajira kupitia mifumo ya kiteknolojia kwa kuratibu, kuomba, na kufanya malipo ya huduma za kilimo mtandaoni.
Vilevile, uzinduzi wa Mkakati wa Pili wa Taifa wa Zana za Kilimo wa Mwaka 2025/2026 hadi 2035/2036 uliofanywa na Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba unaleta matumaini mapya ya ajira endelevu.
Katika upande wa miundombinu, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imekamilisha miradi 28 inayohusisha skimu mpya na ukarabati wa mabwawa, hatua inayoruhusu kilimo kufanyika kipindi chote cha mwaka mzima na kuwapo kwa ajira za kudumu badala ya zile za msimu.
Jitihada hizi funganishi zimeenda mbali zaidi kwa ununuzi wa pampu 1,000 za umwagiliaji zilizosambazwa maalum kwa vikundi vya wakulima wanawake na vijana wa maeneo ya pembezoni mwa Ziwa Victoria na Tanganyika, maeneo ambayo mara nyingi yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za kiuchumi na ukosefu wa fursa.
Kupitia utafiti wa mbegu bora ambapo aina 30 za mbegu za kimkakati zimefanyiwa kazi, uzalishaji wa miche ya ruzuku zaidi ya milioni 37, pamoja na uanzishwaji wa Wakala ya Taifa wa Huduma za Ugani Kilimo inayotarajiwa kuanza Julai Mosi mwaka huu, serikali inajenga mazingira imara yatakayofanya kilimo kuwa chanzo kikuu cha kipato.
Hatua hizi za mageuzi ya kilimo ndiyo mwarobaini wa hoja ya Jaji Chande, kwani zinamtoa kijana mtaani na kumpeleka shambani, na hivyo kulinda usalama na utulivu wa taifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464