` MABILIONI YA CSR KUTOKA BARRICK BULYANHULU KUTEKELEZA MIRADI YA KIJAMII HALMASHAURI YA MSALALA 2026

WANDAMAN HOTEL

MABILIONI YA CSR KUTOKA BARRICK BULYANHULU KUTEKELEZA MIRADI YA KIJAMII HALMASHAURI YA MSALALA 2026

       


Meneja Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Bw. Agapith Paul wa pili kushoto akibadilishana hati ya mkataba na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala , Bw. Mibako Mabubu na wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Nico Kayange.
Meneja Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Bw. Agapith Paul wa pili kushoto akibadilishana hati ya mkataba na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala , Bw. Mibako Mabubu na wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Nico Kayange.
Meneja Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Bw.  Agapith Paul akisaini mkataba wa makubaliano ya kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia sheria , kanuni za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Nico Kayange akiweka saini kwenye makubaliano hayo , katikati ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala , Bw. Mibako Mabubu akishuhudia.
Afisa Mahusiano ya Jamii Mwandamizi wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu , Zuwena Senkondo akitia saini kwenye mkataba huo.
Afisa Mahusiano ya Jamii Mwandamizi wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu , Zuwena Senkondo akizungumza kwenye halfa hiyo.

***
Uwekezaji wa kampuni ya Barrick nchini yenye ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga unazidi kuleta manufaa ambapo mwaka huu mgodi wa Barrick Bulyanhulu umetoa kiasi cha shilingi bilioni 1.8 za uwajibikaji kwa jamii kwa Halmashauri ya wilaya ya Msalala kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali 26 ya maendeleo kwa wananchi.

Hafla ya utiliaji saini mkataba huo wa ushirikiano kupitia CSR imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo ambapo ulishuhudiwa na viongozi mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala na Wafanyakazi wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala , Bw Mibako Mabubu amesema fedha hizo zitaelekezwa kwenye miradi 26 ya jamii ya Afya , Elimu, Miundombinu na Uwekezaji.

Mabubu pamoja na mambo mengine ametoa wito kwa Madiwani na Watalaamu wa Halmashauri hiyo kuwatangazia wananchi miradi hiyo inayotekelezwa na fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Mgodi wa Barrick Bulyanhulu ili waweze kukuza uelewa wao kuhusu manufaa ya kuwepo kwa mgodi huo kwenye Halmashauri yao.

“Hakikisheni mnafanya mikutano ya hadhara kwa wananchi kwenye kata zenu kwa ajili ya kuzungumzia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kupitia sheria na kanuni ya CSR ili wananchi waelewe faida ya kuwa na mgodi huu”, amesisitiza.

Kwa upande wake , Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Nico Kayange amesema ufanisi wa miradi inayotekelezwa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kupitia fedha za CSR ni mkubwa na una matokeo chanya kwa jamii.

“Sehemu kubwa ya utekelezaji wa miradi ya kijamii kwenye wilaya yetu imejikita kwenye mahitaji na vipaumbele vya wananchi husika na kila mwaka maendeleo na ufanisi kwa miradi hii ni ya kuridhisha sana,” ameongeza.

Amesema pamoja na mambo mengine lakini utekelezaji wa miradi ni shirikishi ili wananchi husika waweze kuibua mahitaji na vipaumbele vyao kwenye kata husika.

“Tunatekeleza miradi kupitia mpango shirikishi na hatufanyi kama Halmashauri – bila kukusanya na kupata mawazo ya wananchi na madiwani ambao ndio wawakilishi wao na maelekezo ni kwamba mipango yote ijikite katika kutatua kero za wananchi na vipaumbele vyao,” amesisitiza Kayange.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja Mgodi wa Barrick Bulyanhulu , Meneja Mahusiano ya Jamii, Bw Agapith Paul amesema kuwa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu utaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha fedha za CSR zinazotolewa na mgodi huo kila mwaka zinaendelea kuwaletea maendeleo wananchi na kuboresha maisha yao ili wanufaike na uwekezaji wa mgodi huo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464