
Katibu wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Shinyanga mjini Doris Kibabi akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa kata ya Masekelo baada ya kupanda miti ya matunda katika shule ya sekondari Masekelo
Na Suzy Butondo,Shinyanga press blog
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Shinyanga mjini, Doris Kibabi, amekemea vikali vitendo vya uvutaji bangi na unywaji pombe kwa wanafunzi wa shule za sekondari wilayani humo, akiwataka wajikite katika masomo ili waweze kutimiza ndoto zao.
Mbali na kukemea vitendo hivyo, amewataka pia wanafunzi wa kiume kukataa kushawishiwa na wanawake wanaojulikana kama “mishangazi”, ambao huwavutia vijana kwa kuwapa fedha na baadaye kuwaingiza katika mienendo isiyofaa.
Kibabi ametoa kauli hiyo leo wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Jumuiya ya Wazazi, yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Masekelo, iliyopo Manispaa ya Shinyanga, ambapo pia walipanda miti ya matunda. Aliwasisitiza wanafunzi wote kusoma kwa bidii na kujiepusha na matumizi ya pombe, bangi na mahusiano yasiyofaa.
Aidha, alizungumza na wanafunzi pamoja na wazazi wa Kata ya Masekelo, akiwahimiza wazazi kushirikiana na walimu katika kusimamia nidhamu na maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao, huku wakiwafundisha maadili mema.
“Niwaombe wanafunzi wa Masekelo na kata nyingine za wilaya hii kuzingatia masomo. Msikubali kushawishika na mambo yasiyofaa yanayopoteza muda wenu. Epukeni matumizi mabaya ya simu na mitandao ya kijamii, kwani baadhi ya maudhui yanaweza kuwaharibu na kuwaingiza katika vitendo visivyofaa,” amesema Kibabi.
Pia amewataka wazazi kuacha kuwatuma watoto kupeleka zawadi kwa mahusiano ya pembeni (“michepuko”), akisema tabia hiyo inachangia kuwaharibu watoto na kuwafanya waige mienendo mibaya. Aliwasihi wazazi kuzingatia maadili ya Kitanzania.
“Ni muhimu wazazi kuhudhuria vikao vya shule wanapoitwa na walimu, pamoja na kuchangia chakula shuleni ili kusaidia watoto kusoma kwa utulivu na kufaulu. Pia msikubali zawadi wanazowaletea watoto, kwani kufanya hivyo kunawahamasisha kuendelea kushawishika na vitendo visivyofaa,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Kibabi alisema Jumuiya ya Wazazi imetoa cheti cha pongezi kwa walimu wa Shule ya Sekondari Masekelo kwa kushika nafasi ya tatu kiwilaya na kimkoa, akiwapongeza kwa juhudi zao za kuinua kiwango cha ufaulu.
“Tunampongeza mwalimu mkuu na walimu wote kwa kazi kubwa waliyoifanya. Hapo awali shule hii ilikuwa na sifa mbaya, lakini sasa imepiga hatua kubwa kitaaluma,” alisema.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji, Daniel Kapaya, aliwataka wanafunzi kuepuka kubeba simu shuleni, akieleza kuwa baadhi ya matumizi ya mitandao huwapotosha. Aliwashauri kuwa na subira hadi watakapofikia umri sahihi wa kutumia teknolojia hizo kwa manufaa.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Masekelo, Anthon Venance Mlowe, aliishukuru Jumuiya ya Wazazi kwa kuwapatia cheti cha pongezi na kuahidi kuendeleza juhudi za kuongeza ufaulu na kuondoa kabisa daraja la nne na sifuri.
Aidha, alitoa rai kwa walimu kutumia nidhamu stahiki kwa wanafunzi bila kutumia adhabu kali kupita kiasi.
Katibu wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Shinyanga mjini Doris Kibabi akizungumza na wazazi wenye watoto katika shule ya sekondari Masekelo



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464