.mp4.00_00_21_14.Still007.jpg)
Katika kuimarisha harakati za kuhubiri amani na mshikamano wa kijamii, Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Mkoani Shinyanga imeanzisha kamati ndogo ndogo 17 zitakazosaidia kusimamia na kuratibu shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo ndani ya mkoa huo.
Mwenyekiti wa JMAT
Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Balilusa Khamis, amesema hatua ya kuunda kamati hizo
inalenga kuongeza ufanisi wa utendaji kazi pamoja na kuhakikisha jumuiya hiyo
inawafikia wananchi wengi zaidi kupitia elimu ya amani, maridhiano na upendo.
Amesema kamati
hizo zitakuwa na jukumu la kuratibu shughuli mbalimbali zinazohusu kuimarisha
mshikamano wa kijamii, kuhamasisha maadili mema na kuendelea kujenga mazingira
ya utulivu na ushirikiano miongoni mwa Watanzania.
Sheikh Balilusa ameongeza kuwa JMAT itaendelea
kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha jamii inaendelea kuishi kwa amani
na kuheshimiana bila kujali tofauti zao za kidini, kisiasa au kijamii.
Sheikh Balilusa amesema suala la
maridhiano na amani ni jambo muhimu katika maisha ya kila mwananchi na
kusisitiza kuwa jumuiya hiyo haibagui dini, kabila wala mila kwani imekusanya
viongozi wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wa kimila kwa lengo la kujenga
umoja wa kitaifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Baraza la Wazee Manispaa ya Shinyanga, Stephano Tano amesema Watanzania
wanapaswa kuendelea kushikamana katika kulinda umoja wa taifa kama
alivyoelekeza Hayati Julius Nyerere kuwa ulinzi wa taifa ni jukumu la kila mtanzania
mzalendo.
Naye mjumbe wa kamati ya JMAT, Anna
Mwalongo amesema amani ndiyo msingi wa maisha bora na maendeleo ya jamii,
akieleza kuwa mali, familia na mafanikio yote hayana maana ikiwa hakuna amani
nchini.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kulinda tunu za taifa kwa kudumisha upendo, mshikamano na maridhiano ili kuendelea kuijenga Tanzania yenye umoja na utulivu.
.mp4.00_00_17_00.Still008.jpeg)
.mp4.00_00_28_17.Still006.jpeg)
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464