` WATANZANIA WAHIMIZWA KUSAHAU YALIYOPITA NA KUJENGA TAIFA KWA UMOJA

WANDAMAN HOTEL

WATANZANIA WAHIMIZWA KUSAHAU YALIYOPITA NA KUJENGA TAIFA KWA UMOJA

 

Watanzania wametakiwa kusahau yaliyopita na kuelekeza nguvu zao katika kujenga taifa lenye mshikamano, upendo na maendeleo ya pamoja. Wito huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya kuimarisha umoja wa kitaifa na kuhakikisha nchi inaendelea kusonga mbele kwa amani na utulivu.

Imeelezwa kuwa kushikilia mambo ya zamani kunachangia kudhoofisha mshikamano wa jamii na kuzuia juhudi za maendeleo, badala yake wananchi wanapaswa kuunganisha nguvu zao na kuangalia mustakabali wa taifa kwa mtazamo chanya unaolenga ustawi wa wote.

 Wito huo umetolewa na mwanasiasa Abdalla Sube mkazi wa Manispaa ya  Shinyanga, amewaomba watanzania kuendeleza upendo miongoni mwao bila kujali tofauti za rangi, dini au makabila,kwani taifa lenye watu wanaothaminiana na kuheshimiana ndilo linaloweza kufikia maendeleo endelevu.

Pia amebainisha kuwa ubaguzi wa aina yoyote unaweza kuwa chanzo cha migogoro na kuvuruga amani iliyopo, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kulinda na kuimarisha mshikamano wa kitaifa kwa vitendo.

Amesema watanzania tunatakiwa kushikamana, kupendana na kusonga mbele kwa lengo la kuijenga nchi imara yenye umoja, amani na maendeleo kwa kizazi cha sasa na kijacho na kusau mambo yaliyotokea nyuma.

Amesisitiza umoja na upendo  kuwa ni msingi muhimu katika kuleta maridhiano ya kweli ndani ya Jamii, wananchi wanapaswa kujenga tabia ya kusameheana, kusikilizana na kuheshimiana ili kuondoa tofauti zinazoweza kuleta migawanyiko.

Kupitia mshikamano huo, jamii inaweza kurejesha imani na kuimarisha uhusiano mzuri unaochochea maendeleo ya pamoja na kujenga taifa linalozingatia utu na kuleta maridhiano kwa pande zote.

Amesisitiza kuwa maridhiano ya kudumu hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa moyo wa upendo na nia ya dhati ya kuishi kwa amani,kwa kuzingatia misingi ya utu na kushirikiana katika shughuli za kijamii na kiuchumi bila kubaguana, hali hiyo itasaidia kujenga taifa lenye utulivu, mshikamano na lenye mwelekeo wa maendeleo endelevu.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464