
KATIKA kipindi hiki ambacho Tanzania inapita kwenye daraja muhimu la kutafuta amani ya kudumu, maridhiano na umoja wa kitaifa, vijana wametakiwa kutambua kuwa wao ndio "jeshi" la kwanza la kulinda utulivu huo kupitia uzalishaji mali na matumizi ya teknolojia.
Rai hiyo imetolewa kama sehemu ya mkakati wa kuhakikisha vijana hawawi vishawishi vya uvunjifu wa amani, bali wanakuwa chimbuko la suluhu na maendeleo.
Akizungumza kwa mamlaka juu ya mustakabali wa vijana katika enzi hii ya sayansi na teknolojia, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Kizumbi, John Mwela, amebainisha kuwa kijana asiyejishughulisha ni hatari kwa usalama wa nchi.
Amesema kuna haja ya haraka ya kuwa na mpango mkakati utakaowawezesha vijana kujitegemea na kuwajibika, jambo ambalo ndilo msingi mkuu wa kuimarisha umoja na upendo miongoni mwa Watanzania.
Amani Inajengwa na Kijana Anayejituma
Mhadhiri Mwela amesisitiza kuwa maridhiano ya kweli na umoja wa kitaifa hayawezi kupatikana ikiwa nguvu kazi kubwa ya taifa (vijana) itabaki nyuma bila kujitambua. Amesema Serikali imeshafungua milango na kuweka mazingira "super" rafiki, hivyo vijana wanapaswa kuingia uwanjani na kuzichamgamkia fursa hizo ili kujenga mustakabali wao na wa nchi.
"Huwezi kuwa na amani ya dhati kama kijana hajishughulishi. Lazima tubadili mtazamo; nchi ina fursa nyingi na hatuhitaji vijana wanaolalamika na kusubiri ajira rasmi, bali tunahitaji 'mashujaa' wa kiuchumi watakaoitumia sayansi na teknolojia kujikwamua," alisema Mwela.
Uzalendo na Sayansi: Silaha ya Utulivu
Pamoja na msisitizo wa kiuchumi, ujumbe mzito umetolewa kuhusu uzalendo. Vijana wametakiwa kuwa walinzi wa kwanza wa utulivu na mshikamano wa kitaifa. Mwela amebainisha kuwa katika dunia ya sasa ya kidijitali, vijana wanapaswa kutumia maarifa yao na ubunifu kama zana ya kuunganisha taifa badala ya kuligawa.
Amesema kuwa kasi ya mabadiliko ya dunia inahitaji vijana wenye akili za kisasa ambao wanaweza kuendana na sayansi na teknolojia, Hivyo, kujifunza kwa bidii na kuongeza ubunifu ni wajibu usiopingika kwa kijana yeyote anayeitakia heri Tanzania.
Wito wa Hatua
Mwela alisisitiza kuwa ipo haja ya elimu inayopatikana sasa lazima itafsiriwe kwa vitendo vya uzalishaji mali akihimiza kutumia elimu hiyo kama ufunguo wa kujitegemea, wakitambua kuwa wao ndio mhimili mkuu wa maridhiano na amani ya kweli kwa kuacha kuwa watazamaji na kuwa washiriki wakamilifu katika kuijenga Tanzania yenye umoja, utulivu na neema kwa kila mmoja.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464