` UZALENDO NA AMANI NI MSINGI WA MAENDELEO YA TAIFA

WANDAMAN HOTEL

UZALENDO NA AMANI NI MSINGI WA MAENDELEO YA TAIFA

 

Mkazi wa Kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga, Abdalla Sube ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha uzalendo, amani na utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa mambo hayo ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.

Sube amesema kuwa uzalendo wa kweli unapaswa kuanzia kwa kila mwananchi kutimiza wajibu wake, kuheshimu sheria za nchi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Ameeleza kuwa bila uzalendo, ni vigumu kwa taifa kufikia malengo yake ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, amebainisha kuwa amani na utulivu vilivyopo nchini vimekuwa chachu ya maendeleo katika sekta mbalimbali, zikiwemo biashara, kilimo na uwekezaji, hali inayowezesha wananchi kufanya kazi zao kwa uhuru na ufanisi.

Ameongeza kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kulinda na kuenzi amani iliyopo, kwani kuvurugika kwa hali ya usalama kunaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa ustawi wa jamii na uchumi wa nchi kwa ujumla.

 Amesema kuwa mshikamano miongoni mwa wananchi ni nguzo muhimu inayoweza kusaidia kudumisha amani, huku akisisitiza kuwa tofauti za kiitikadi, kidini au kikabila hazipaswi kuwa chanzo cha migogoro.

Amewaomba  watanzania kuendelea kuliombea taifa na kuendeleza moyo wa uzalendo ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na yenye maendeleo endelevu.

Abdalla Sube amewataka vijana kujiepusha na vitendo vya vurugu vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi, amesema vijana wana nafasi kubwa katika ujenzi wa taifa, hivyo wanapaswa kutumia nguvu zao katika shughuli za maendeleo badala ya kushiriki katika matendo yanayoweza kuvuruga utulivu uliopo.

Amehitimisha kwa kueleza kuwa  ni muhimu kwa vijana kuwa na nidhamu, kujitambua na kuzingatia sheria za nchi, huku wakiepuka kushawishiwa kujiingiza katika migogoro isiyo na tija hivyo wanapaswa kuwa mfano mzuri kwa kulinda amani na kuendeleza uzalendo kwa vitendo.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464