` SERIKARI YAOMBWA KUWAHI KUOKOA WATOTO WANAOTESEKA KUTAFUTA ELIMU

WANDAMAN HOTEL

SERIKARI YAOMBWA KUWAHI KUOKOA WATOTO WANAOTESEKA KUTAFUTA ELIMU


Meya wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza

Na Suzy Butondo Shinyanga


Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Busambilo, uliopo katika Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga, wameiomba serikali kuwasaidia kukamilisha ujenzi wa shule ya msingi ili kuwaondolea adha ya watoto wao kutembea umbali mrefu kufuata elimu.

Wananchi hao wamesema kuwa kwa sasa wanafunzi wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita tano kwenda kusoma katika maeneo ya jirani.

Mkazi wa Busambilo, Christina Bunzali, amesema kuwa shule inayotumiwa kwa sasa ipo umbali wa zaidi ya kilomita tano kutoka mtaa huo kuelekea eneo la Mwalugoye, nje kidogo ya Manispaa ya Shinyanga.

“Tunaiomba serikali itusaidie, watoto wetu wanapata shida sana kwa kutembea umbali mrefu kufuata elimu, tunaomba tujengewe shule katika eneo letu ili waweze kusoma vizuri,” amesema Christina.

Naye Mathias Mauge, mkazi wa mtaa huo, amesema umbali huo ni changamoto kubwa kwa wanafunzi, kwani hulazimika kuamka mapema sana na wakati mwingine hukumbana na hatari njiani.

“Watoto wanaamka mapema sana, hata saa 11 alfajiri, na wako kwenye hatari ya kufanyiwa vitendo viovu njiani,” amesema Mauge.

Kwa upande wake, Sara Masunga amesema baadhi ya watoto hulazimika kuacha shule kutokana na umbali huo.

“Watoto wengine wanaacha shule kwa sababu ya umbali. Tulikubaliana kuchangia shilingi 15,000 kila mmoja kwa ajili ya ujenzi wa shule, lakini hali ngumu ya maisha imesababisha wengi kushindwa kuchangia. Tunaomba serikali itusaidie,” amesema Sara.


Mwenyekiti wa kitongoji cha Busambilo, kata ya Chibe, Julius Juma, amesema ni kweli hakuna shule ya msingi katika eneo hilo, na watoto hulazimika kusoma katika shule za Mwamapalala na Chibe zilizo umbali wa kilomita tano hadi sita.

“Tulikaa na wananchi na kukubaliana kuchangia shilingi 15,000 kila mmoja, lakini wengi wameshindwa kutokana na hali ngumu ya maisha. Hadi sasa tumekusanya zaidi ya shilingi laki nne tu, tunaomba serikali itusaidie ili watoto wetu wasiendelee kupata shida,” amesema Juma.


Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Salum Kitumbo, amesema tayari manispaa imebaini changamoto hiyo na imeanza mchakato wa ujenzi wa shule katika eneo la Busambilo,
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ina mkakati wa kuhakikisha maeneo yote yanakuwa na shule bora na watoto wanasoma katika mazingira mazuri,” amesema Kitumbo.

Ameongeza kuwa wamefanya mashauriano na madiwani  ili kuhakikisha maeneo yote yenye umbali wa zaidi ya kilomita tatu katika manispaa ya Shinyanga yanapatiwa shule.

“Hatutaki wanafunzi watembee umbali mrefu. Tunatambua umuhimu wa elimu, hivyo hili ni miongoni mwa vipaumbele vyetu,” ameongeza.

Aidha, Kitumbo amesema manispaa inaendelea kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyokuwa ikisuasua, ikiwemo ujenzi wa soko kuu, pamoja na kuboresha soko la mbao la Chamaguha.












Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464