` RAFIKI SDO, SAVE THE CHILDREN YAWANOA VIONGOZI KUWASHIRIKISHA WATOTO VIKAO VYA MAAMUZI

WANDAMAN HOTEL

RAFIKI SDO, SAVE THE CHILDREN YAWANOA VIONGOZI KUWASHIRIKISHA WATOTO VIKAO VYA MAAMUZI

 

RAFIKI SDO, SAVE THE CHILDREN YAWANOA VIONGOZI KUWASHIRIKISHA WATOTO VIKAO VYA MAAMUZI

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

VIONGOZI mbalimbali ngazi ya Halmashauri na Kata katika Manispaa ya Shinyanga, wameeleza kufaidika na mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kushirikisha watoto katika vikao vya maamuzi, hatua inayolenga kuhakikisha vipaumbele vyao vinaingizwa kwenye mipango ya bajeti.

Wamebainisha hayo leo Aprili 22, 2026, wakati wa mafunzo ya uwajibikaji kwa viongozi, yanayozingatia maslahi na ushirikishwaji wa watoto, yaliyoandaliwa na Shirika la Rafiki SDO kwa kushirikiana na Save the Children.
Mratibu wa Baraza la Watoto Manispaa ya Shinyanga Kashinje Shija, amesema mafunzo hayo yataongeza ushirikishwaji wa watoto katika masuala yanayowahusu moja kwa moja, ikiwamo utoaji wa vipaumbele vitakavyoingizwa kwenye bajeti za Halmashauri.

“Mafunzo haya yatasaidia kuhakikisha watoto wanashirikishwa kikamilifu kwenye vikao vya maamuzi, ili waweze kutoa vipaumbele vyao, na hatimaye viingizwe kwenye mipango ya bajeti,” amesema Shija.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga Kabula Michael, amesema baada ya mafunzo hayo watakuwa wakishirikisha mabaraza ya watoto katika vikao vya maamuzi ngazi ya kata, hususan wakati wa maandalizi ya mipango ya bajeti.
Amesema, hatua hiyo itasaidia kubaini mahitaji yao halisi ya watoto, na kuyajumuisha katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ikiwamo ya maendeleo.

Kwa upande wake, Afisa Mipango wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Gabriel Walinguzo, amesema ushirikishwaji wa watoto utawezesha kutengwa kwa bajeti inayolenga mahitaji yao halisi.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO, Gerald Ng’ong’a, amesema awali waliwajengea uwezo watoto kupitia mabaraza yao kuhusu namna ya kushiriki katika vikao vya maamuzi, na sasa wameelekeza nguvu kwa viongozi, ili kuhakikisha wanawashirikisha watoto ipasavyo kwenye vikao ambavyo vinahusu mambo yao.

Amesema, hatua hiyo inalenga kuhakikisha maoni ya watoto yanazingatiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya namba 21 ya mwaka 2009.
Viongozi waliopewa mafunzo hayo ni Wenye viti wa Mtaa, Afisa Ustawi wa Jamii, Diwani, Afisa Maendeleo, Mtendaji wa Kata, Afisa Elimu Msingi na Sekondari, Afisa Elimu Maalumu, Mratibu wa Baraza la watoto na Afisa Mipango.

MAELEZO KATIKA PICHA NA VIDEO KWA CHINI👇👇
Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO Gerald Ng'ong'a akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO Gerald Ng'ong'a akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mratibu na Utawala haki za watoto kutoka Shirika la Save The Children Victor Mukiza akiendelea na utoaji wa mafunzo kwa viongozi.
Mafunzo yakiendelea.

TAZAMA VIDEO HAPA CHINI👇👇


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464