Mwenyekiti wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania (VIWAWA), Leonard Mapolu, amewahimiza vijana nchini kuthamini na kulinda amani iliyopo pamoja na kuuenzi muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akisisitiza kuwa ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa.
Mapolu amesema kuwa muungano huo ni alama ya mshikamano wa Watanzania na unapaswa kulindwa kwa nguvu zote, kwani umekuwa chachu ya maendeleo katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Ameonya kuwa jitihada zozote za kuvuruga amani zinapaswa kupuuzwa na kukemewa kwa pamoja kwani wanaofanya hivyo hawana nia njema na wanapaswa kupuuzwa.
Akizungumzia suala la amani, Mapolu alieleza kuwa amani inaanza kwa mtu binafsi katika maisha ya kila siku, hususan katika utoaji wa huduma. Alisisitiza kuwa kila mmoja anatakiwa kutenda haki kwa wengine ili kuhakikisha mazingira ya utulivu yanaendelea kudumishwa katika jamii.
Aidha, amesema kuwa uzoefu wake wa kuzunguka maeneo mbalimbali ya nchi katika shughuli za utume umemuwezesha kuona namna ambavyo amani ilivyo muhimu katika kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi. Ameeleza kuwa bila amani isingekuwa rahisi kufika na kuhudumia jamii katika maeneo mbalimbali.
Mapolu amewasihi vijana kutambua nafasi yao kubwa katika kulinda amani ya nchi, akisema kuwa wao ni nguvu kazi ya taifa na wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha utulivu unaendelea kudumu. Amewatahadharisha vijana dhidi ya kutumika vibaya na watu wenye nia ya kuvuruga amani.
Kwa upande mwingine, amesisitiza umuhimu wa vijana kujenga mshikamano, kuheshimiana na kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii. Ameeleza kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji utulivu na ushirikiano wa wananchi wote pamoja na maridhiano.
Akihitimisha, Mapolu ametoa wito kwa vijana na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuilinda amani ya nchi kwa nguvu zote, akibainisha kuwa amani ni tunu adhimu inayopaswa kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464