Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mkoa wa Shinyanga umetajwa kuwa mwenyeji wa maonyesho ya Tano ya Shirika la Maendeleo na Viwanda Vidogo (SIDO) kitaifa yenye lengo la kuinua uchumi wajasiriamali wadogo, kupitia kujifunza namna ya kuzalisha bidhaa bora na zenye ushindani na kupanua wigo wa mtandao katika biashara zao.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 10, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Mhandisi Prof. Silvester Mpanduji wakati akizungumza na wajasiriamali juu ya maandalizi ya maonyesho hayo.
Amesema, maonyesho hayo yatafanyika katika Manispaa ya Kahama, kuanzia Oktoba 21 hadi 30 mwaka huu, katika Uwanja wa Magufuli, ambayo yatakutanisha wajasiriamali kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini zikiwamo na taasisi za kifedha.
“Maonyesho haya yatakuwa fursa kwa wajasirimali wadogo kwa kuonyesha bidhaa, kujifunza Tecknolojia ya uzalishaji wa bidhaa, kubadilishana uzoefu, kubuni bidhaa mpya na kujenga mtandao wa kibiashara ndani na nje ya nchi,” amesema Mpanduji.
Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga David Lyamongi, amesema mkoa huo wa Shinyanga upo tayari kwa maonyesho hayo, na miundombinu yote ipo, huku akiwahakikishia washiriki kuwa usalama upo wa kutosha.
Amesema, maonyesho hayo ni fursa kubwa kwa wajasiriamali katika mkoa huo, na kutoa wito wajitokeze kwa wingi hasa vijana ili wapate kujifunza vitu mbalimbali ikiwamo namna ya kujiajiri, kupata mitaji na hata kufungua viwanda vidogo.
Naye Mmoja wa Wajasiriamali hao Sylivia Sylivery, amesema maonyesho hayo ni fursa kwao kujitangaza kwa kuonyesha bidhaa zao, kupata uzoefu, kujifunza namna ya kuzalisha bidhaa bora pamoja na kujenga mtandao wa kibiashara.
MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo na viwanda vidogo (SIDO) Mhandisi Prof. Silvester Mpanduji akizungumza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464













