Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MADEREVA watatu mkoani Shinyanga wamefungiwa leseni zao kwa kipindi cha miezi mitatu kila mmoja, baada ya kukutwa wakiendesha kwa mwendo kasi zaidi ya kilomita 80 kwa saa.
Hayo yamebainishwa leo na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Jeneth Magomi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia operesheni walioifanya mwenzi machi mwaka huu.
RPC MAGOMI.
Amesema, kwa kipindi hicho wamekamata jumla ya mkosa 5,648 ya usalama barabarani, makosa ya magari yalikuwa 4,044, ya bajaji na pikipiki 1,604, huku wahusika wakiwajibishwa kwa kulipa faini papo ya kwa hapo.
“Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha usalama barabarani tumewafungia leseni madereva watatu kwa muda wa miezi mitatu kwa kosa la kuendesha gari mwendokasi zaidi ya kilomita 80 kwa saa,” amesema Magomi.
Katika tukio jingine, mwanamke aliyefahamika kwa jina la Hollo Ruchanganya (60), mkazi wa Kijiji cha Bunambiyu wilayani Kishapu, ameuawa kwa kuchinjwa na mtu anayedaiwa kuwa mgeni aliyefika nyumbani kwake akitafuta mganga wa jadi.
Magomi alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku katika kijiji hicho, ambapo mtu huyo alifika nyumbani kwa marehemu akijitambulisha kuwa anatoka Kijiji cha Sanga wilayani Kwimba, akihitaji kupelekwa kwa mganga wa jadi anayejulikana kwa jina la Ng’wana Masanja ambaye ni mama mdogo wa marehemu.
Amesema marehemu alimpeleka mgeni huyo kwa mganga huyo, lakini tangu alipomsindikiza hakurejea tena nyumbani, na baadaye mwili wake ulikutwa shambani akiwa amefariki dunia, na uligunduliwa na ndugu yake alipokuwa akielekea shambani.
“Tunawashikilia watu wawili, ambao ni mganga na msaidizi wake kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo kwa ajili ya mahojiano, huku tukimtafuta mgeni aliyekuwa na marehemu, tukio hili linahusishwa na imani za kishirikina,” amesema Magomi.
Aidha, amesema katika operesheni hiyo, jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 35, wakiwamo wanane wanaodaiwa kuhusika na wizi wa vifaa mbalimbali kwenye ujenzi wa reli ya mwendokasi (SGR).
Amevitaja vifaa vilivyokamatwa kuwa ni vipande 306 vya nondo, mabomba 32 ya milimita 12, stendi 12 za makarasha na mabomba ya mraba 65.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu, huku akiwahimiza wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao katika kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka.
Amesema, Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa, hususan katika maeneo ya ibada.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464