` AMANI NA UTULIVU NDIO INJINI YA MAGEUZI YA KIUCHUMI KWA WAFUGAJI NA VIJANA NCHINI

WANDAMAN HOTEL

AMANI NA UTULIVU NDIO INJINI YA MAGEUZI YA KIUCHUMI KWA WAFUGAJI NA VIJANA NCHINI

Wafugaji katika Manispaa ya Shinyanga wamesisitiza kuwa amani na utulivu ndio mhimili mkuu unaowawezesha kufanya shughuli zao kwa uhuru na kukuza kipato kinachochangia ustawi wa maisha yao na pato la taifa kwa ujumla. 

Katika mahojiano maalumu, wafugaji hao wamebainisha kuwa fursa lukuki zilizopo kwenye sekta ya mifugo zinaweza tu kutumika kikamilifu ikiwa nchi itaendelea kuwa na utulivu, jambo linalotoa mwanya kwa vijana kuachana na vijiwe na badala yake kujikita kwenye ufugaji wa kisasa kama njia ya kujiajiri. 

Kwa kuitazama amani kama mtaji, wafugaji hao wanaamini kuwa kijana mwenye shughuli ya tija anakuwa mlinzi namba moja wa mshikamano wa kitaifa kwa kuwa anaona hatima ya maisha yake ikiwa katika mikono salama.

Mmoja wa wafugaji hao, John Bigabo, ametoa wito kwa vijana kote nchini kuchangamkia fursa za ufugaji ili kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa nchi, huku akisisitiza kuwa utulivu uliopo sasa nchini unawapa nafasi ya kutoa ajira na kuleta mabadiliko ya kimaisha kwa jamii inayowazunguka.

 Aidha, imeelezwa kuwa wakati Tanzania ikitekeleza kampeni ya kuimarisha maridhiano na mshikamano wa kitaifa, kundi la vijana linapaswa kuelimishwa na kupewa ujuzi wa kibiashara ili kuendesha miradi yenye tija itakayowaepusha na vishawishi vinavyoweza kuvuruga utulivu wa nchi. 

Mazingira haya ya utulivu yanajenga matumaini na kuimarisha imani ya wananchi kwa serikali yao ambayo inaendelea kuweka sera rafiki na kutoa mikopo pamoja na huduma za ugani kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Naye mfugaji Yohana Jacob amebainisha kuwa sekta ya mifugo ina soko kubwa linalohitaji nguvu kazi ya vijana wenye mtazamo chanya, ambapo kuongezeka kwa ajira katika sekta hiyo ni chachu ya kudumisha amani na mshikamano miongoni mwa wananchi.

 Alihimiza vijana kuachana na fikra potofu kuwa ufugaji ni kazi ya duni na badala yake waione kama fursa ya kisasa inayoweza kuwatoa kwenye changamoto za kiuchumi na kuwafanya waishi kwa heshima na amani. 

Kupitia mshikamano wa kiuchumi na maridhiano ya kijamii, wafugaji hao wanaamini kuwa Tanzania itasonga mbele kwa kasi zaidi kwani amani inapotawala, kila mwananchi anapata utulivu wa akili wa kubuni na kutekeleza malengo yake ya kimaisha kwa mafanikio makubwa. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464