` VIJANA WAZIDI KUKWEA KATIKA DIPLOMASIA YA TANZANIA, DIANA CHANDO KUONGOZA AGENDA YA AMANI

WANDAMAN HOTEL

VIJANA WAZIDI KUKWEA KATIKA DIPLOMASIA YA TANZANIA, DIANA CHANDO KUONGOZA AGENDA YA AMANI

Uteuzi wa vijana wa Kitanzania katika nafasi za juu za kimataifa umezidi kushika kasi baada ya Diana Chando kuteuliwa kuwa Mkuu wa Utawala, Amani na Ulinzi katika Jukwaa la Vijana la Kusini mwa Afrika (SAYoF). 

Jukwaa hili, linalofanya kazi chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ni kiungo muhimu kinachounganisha vijana wa nchi za ukanda huu katika kukuza uongozi, utawala bora, pamoja na usalama wa kikanda.

Diana, ambaye ni mwanadiplomasia mbobezi, anakuja na uzoefu mpana katika masuala ya utawala na maendeleo endelevu. 

Akiwa na elimu ya Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo Endelevu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pamoja na Shahada ya Sheria na Mahusiano ya Kimataifa, wasifu wake unaakisi uwezo mkubwa wa kiushindani katika nyanja za sera na ushirikiano wa kimataifa.

Safari yake ya uongozi imepambwa na mafanikio makubwa, ikiwemo kuhudumu kama Balozi wa Vijana wa Umoja wa Afrika (AU) katika Idara ya Ulinzi na Usalama akiziwakilisha nchi 14 za Afrika Mashariki. 

Utambuzi wake kimataifa ulifikia kilele mwaka 2023 alipotajwa miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa wenye asili ya Afrika (MIPAD), na baadaye mwaka 2024 kujumuishwa kwenye orodha ya wanawake mashuhuri barani Afrika, hatua inayothibitisha uwezo wake wa kiuongozi na kimkakati.

Kupitia nafasi hii mpya ndani ya SAYoF, Diana Chando anatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika kuimarisha sauti na ushiriki wa vijana kwenye mifumo ya maamuzi ya SADC. 

Jukumu lake litakuwa kielelezo cha jinsi vijana wa Kitanzania wanavyoweza kuchangia katika kukuza amani, usalama, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika ukanda wa Kusini mwa Afrika na bara zima kwa ujumla. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464