Zoezi la pamoja la medani la 'Justified Accord 2026', lililohusisha Kikosi Maalum cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Kikosi cha Jeshi la Marekani cha Walinzi wa Taifa kutoka Nebraska, limehitimishwa rasmi Machi 12,2026 katika Kata ya Msata, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Akifunga zoezi hilo, Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi, Meja Jenerali Said Nkambi, amesema kuwa majeshi hayo yameendelea kujijengea heshima na uwezo mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yao kupitia ushirikiano huo wa kimkakati.
Meja Jenerali Nkambi amebainisha kuwa Jeshi la Marekani limekuwa likiendeleza uhusiano mwema na JWTZ kwa kubadilishana uzoefu wa mbinu za medani na utoaji wa huduma za tiba, jambo ambalo limekuwa likijenga mtazamo chanya wa wananchi kuelekea jeshi lao.
Amesema kuwa zoezi la mwaka huu limefanyika kwa mafanikio makubwa, na kwamba tathmini itakayofanyika itasaidia kubaini mapungufu yatakayofanyiwa kazi ili kuboresha maandalizi ya mazoezi yajayo, hususan katika masuala ya sayansi na teknolojia ambapo Marekani ni mshirika muhimu.
Hafla hiyo ya ufungaji imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kijeshi na kiraia, akiwemo Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, na Mkuu wa Kamandi ya Marekani Ulaya Kusini Kazi Maalum Afrika, Meja Jenerali Craig Strong.
Zoezi hilo lililoanza tangu tarehe 23 Februari 2026, lililenga kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na majanga ya asili, kutoa mafunzo ya kupambana na uhalifu wa kimtandao, pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za tiba kwa askari na raia.
Katika hatua nyingine ya kuimarisha ushirikiano huo, Jeshi la Marekani kupitia Kikosi cha Walinzi wa Taifa Nebraska, ambao pia wanaongoza Wakala wa Usimamizi wa Huduma za Dharura jimboni humo (NEMA), limelipatia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania magari tisa ya huduma za dharura.
Msaada huo uliotolewa kupitia Ubalozi wa Marekani unalenga kuongeza nguvu katika uokoaji wa watu wanaoathirika na majanga mbalimbali nchini.
Aidha, wajumbe wa kikosi hicho walipata fursa ya kutembelea Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo ili kujionea namna huduma za tiba zinavyotolewa, ikiwa ni sehemu ya kubadilishana uwezo wa kiutendaji kati ya nchi hizo mbili.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464

