` MAPINDUZI YA TIBA: TANZANIA SASA KITOVU CHA UTALII WA TIBA AFRIKA MASHARIKI

WANDAMAN HOTEL

MAPINDUZI YA TIBA: TANZANIA SASA KITOVU CHA UTALII WA TIBA AFRIKA MASHARIKI

Serikali ya Tanzania imepiga hatua nyingine ya kihistoria katika sekta ya afya baada ya kununua kinu cha nyuklia kwa ajili ya mashine ya PET/CT Scan, uwekezaji unaoifanya nchi kuwa kinara wa teknolojia ya uchunguzi wa saratani katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kinu hicho, kilichogharimu shilingi bilioni 18.7, kimeelezwa kuwa ndicho kikubwa zaidi katika ukanda huu, kikilenga kuleta mapinduzi ya kiuchunguzi na matibabu ya kibingwa ambayo hapo awali yalikuwa yakiwatafuta Watanzania wengi nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dkt. Diwani Msemo, amebainisha kuwa teknolojia hiyo mpya ina uwezo wa kipekee wa kuonyesha shughuli za seli ndani ya mwili. Hali hiyo inawawezesha madaktari bingwa kubaini viashiria vya saratani katika hatua za awali kabisa, jambo ambalo ni mhimili mkuu wa kuponya ugonjwa huo.

Uwekezaji huu unatarajiwa kuongeza ufanisi wa taasisi hiyo mara kumi zaidi. Kwa mujibu wa Dkt. Msemo, uwezo wa kuhudumia wagonjwa utapanda kutoka watu watatu hadi watano kwa siku na kufikia wagonjwa 20 hadi 30 kwa siku, hatua itakayopunguza msongamano na muda wa kusubiri huduma kwa wagonjwa wa ndani na nje ya nchi.

"Tunaishukuru Serikali na Wizara ya Afya kwa hatua hii. Ujio wa kinu hiki ni mkombozi kwani utaimarisha ufanisi wa huduma za uchunguzi na kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya saratani nchini," alisema Dkt. Msemo wakati akizungumzia uwekezaji huo mkubwa.

Mbali na kuokoa maisha ya Watanzania, hatua hii inafungua milango ya Utalii wa Tiba, ambapo sasa wagonjwa kutoka nchi jirani hawatakuwa na sababu ya kwenda nchi za mbali kama India au Uturuki, bali watakuja Tanzania kupata huduma za PET/CT Scan zenye viwango vya kimataifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464