.jpg)
Katika kile kinachoonekana ni muendelezo wa kuhubiri siasa za kistaarabu na maridhiano nchini, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekemea vikali tabia ya baadhi ya wadau wa siasa kuwekeana uhasama, kikieleza kuwa siasa za chuki ni "ushamba" usiopaswa kuwa na nafasi katika Tanzania ya leo.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, wakati akizungumza na wanachama katika kikao cha Shina namba mbili, Tawi la Mashineni, wilayani Magu mkoani Mwanza.
Kihongosi amewakumbusha Watanzania kuwa vyama vya siasa visigeuzwe kuwa kuta za kutenganisha undugu, akisisitiza kuwa thamani ya binadamu ipo kwenye mshikamano wa kijamii na si rangi ya itikadi yake.
"Siasa ya kweli ni watu kushikamana, kupendana, kula pamoja na hata kuoana wa vyama tofauti. Kama vyama vinajenga chuki kati ya CHADEMA, CCM, CUF au CHAUMMA, huo ni ushamba wa kisiasa," alisema Kihongosi kwa msisitizo.
Aliongeza kuwa migogoro ya kisiasa mara nyingi huwaumiza wananchi wa kawaida huku viongozi wakibaki salama, hivyo ni vyema watu wakashikamana kwa misingi ya Utanzania. "Ukifa leo hutazikwa na chama; utazikwa na hawa majirani zako wa mazungumzo. Hawa ndiyo watabeba jeneza lako," alikumbusha kiongozi huyo.
Pamoja na kuhubiri amani, Kihongosi alitumia ziara hiyo kukagua utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ukiwemo ujenzi wa Daraja la Sukuma ambalo ni ukombozi wa usafiri wilayani humo. Mradi huo mkubwa unaotekelezwa na Serikali kupitia TANROADS kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 9.4, unatarajiwa kukamilika ifikapo Aprili 16, 2026.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Eng. Ambrose Pascal, amebainisha kuwa ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 70 pamoja na barabara unganishi ya kilometa 2.3 sasa umefikia asilimia 80.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Kihongosi alisema kuwa kazi ya kuleta maendeleo ya vitendo kwa wananchi ndiyo wajibu mkuu wa CCM na Serikali yake, na kwamba daraja hilo ni kielelezo cha namna kodi za Watanzania zinavyorejea kwao kupitia miundombinu bora.
Ni kweli, siasa isitufanye tuwe maadui. Sisi sote ni abiria wa jahazi moja linaloitwa Tanzania. Tunaposhikamana kwenye amani, ndipo tunapopata utulivu wa kujenga madaraja kama hili la Sukuma. CCM imetoa somo muhimu Magu; maendeleo hayana rangi ya chama, na utu ni mkubwa kuliko kadi ya uanachama.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464