` SAUTI ZA DHAHABU: RAIS SAMIA AFUNGUA UKURASA MPYA WA UTU KWA MAGWIJI BITCHUKA NA ZAHIR ZORRO

WANDAMAN HOTEL

SAUTI ZA DHAHABU: RAIS SAMIA AFUNGUA UKURASA MPYA WA UTU KWA MAGWIJI BITCHUKA NA ZAHIR ZORRO

Katika ulimwengu wa muziki wa dansi nchini Tanzania, majina ya Hassan Bitchuka na Zahir Zorro si majina ya kawaida. Hizi ni tunu za taifa; ni sauti zilizobeba huzuni, furaha, na mafundisho ya jamii ya Kitanzania kwa zaidi ya miongo minne.

Wiki hii, tasnia ya sanaa imeshuhudia mguso wa kipekee wa kibinadamu kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye kupitia kwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, amemfikia Hassan Bitchuka nyumbani kwake Sinza Mori, Dar es Salaam.

Hassan Bitchuka, fundi wa mashairi na mwimbaji aliyepata kutamba na bendi za DDC Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’, Msondo Ngoma, na OSS, kwa sasa anapambana na maradhi. Rais Samia amemtumia kiasi cha Shilingi milioni 10 kama mkono wa pole na msaada wa matibabu.

"Rais anathamini mchango usiopimika ambao Bitchuka ametoa kuijenga sanaa ya Tanzania," alisema Mwana FA wakati akikabidhi msaada huo. Hili si jambo dogo; ni ishara kuwa serikali sasa inahamia kwenye falsafa ya "Kazi na Utu"—kutambua kuwa msanii ni binadamu anayehitaji kuthitimiwa wakati wa uhai wake.

Ukitaja Sikinde huwezi kumuacha Bitchuka. Ukitaja darasa la uimbaji lenye weledi, huwezi kumuacha mzee Zahir Zorro. Hawa ni watu walioweka misingi ya muziki wa dansi (Tanzania Rumba) ambao leo hii unarithishwa kwa vizazi vipya.

Bitchuka anajulikana kwa uwezo wake wa kutunga mashairi yenye falsafa nzito na sauti iliyokaa kimamlaka jukwaani wakati Zahir Zorro ni gwiji aliyebobea katika uimbaji wa sauti za juu na uandishi wa nyimbo zinazogusa hisia, huku akiwa ameacha mrithi kama Banana Zorro anayeendeleza kipaji hicho.

Hatua ya Rais kuwakumbuka magwiji hawa, inarejesha heshima ya taaluma ya sanaa ambayo kwa muda mrefu ilionekana kusahaulika pindi wasanii wanapostaafu au kuugua.

Katika mwendelezo huo huo wa kuthamini alama za wasanii, Rais Samia alitumia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kumzawadia mama mzazi wa marehemu Steven Kanumba, Bibi Flora Mtegoa, gari jipya aina ya Harrier (New Model).

Hii ni ujumbe tosha kwa jamii kwamba hata kama msanii ametangulia mbele za haki, alama aliyoiacha (Legacy) bado inatambulika na serikali yake, na familia yake haitaachwa pweke.

Tunapongeza hatua hii ya Rais Samia. Kuwajali magwiji wetu wakati bado wapo nasi ni kitendo cha kishujaa. Inatuma ujumbe kwa wasanii vijana kuwa ukifanya kazi kwa uaminifu na uzalendo, taifa lako litakukumbuka.

Tunamtakia Hassan Bitchuka nafuu ya haraka na tunazidi kuwaombea magwiji wetu wote maisha marefu yenye amani.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464