
Wakati vizabizabina na wapiga kelele wakihangaika kutafuta kasoro zisizokuwepo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya jemadari mahiri, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuchanja mbuga kwa kishindo kuelekea Dira ya Maendeleo ya 2050.
Safari hii, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amezizima kelele hizo huko Hangzhou, nchini China, kwa kunadi fursa kabambe za uwekezaji zinazoifanya Tanzania kuwa "habari ya mjini" duniani kote.
Waziri Kapinga, kwa kujiamini na weledi wa hali ya juu, amewahamasisha miamba wa biashara wa China kuchangamkia fursa kwenye sekta za kimkakati kama viwanda, uongezaji thamani madini, kilimo cha kisasa, na miundombinu.
Hii ni salamu tosha kwa wale wanaodhani serikali imelala; ukweli ni kwamba soko la bidhaa kutoka nchi 33 za Afrika, ikiwemo Tanzania, sasa linaingia China bila ushuru—fursa adhimu kwa wawekezaji kuanzisha viwanda hapa nchini na kutawala masoko ya Afrika na Asia.
Waziri Kapinga ameweka wazi kuwa Tanzania siyo tu kisiwa cha amani, bali ni kitovu cha uchumi kinachokua kwa kasi ya asilimia 7. Kwa wale wanaokebehi juhudi za serikali, takwimu hizi ni jibu tosha:Miradi ya China: Kati ya mwaka 2021 na Desemba 2025, miradi 876 yenye thamani ya dola bilioni 8.8 imesajiliwa nchini.
Ajira: Watanzania zaidi ya laki moja na elfu arobaini na sita (146,000) wamepata ajira kupitia uwekezaji huu wa kishindo wa Awamu ya Sita.
Huku tukielekea Dira ya 2050, Waziri Kapinga amenadi mradi mkubwa wa Bagamoyo Eco Maritime City. Huu siyo mradi wa kawaida; ni mradi utakaogeuza Tanzania kuwa kitovu cha kimataifa cha biashara na viwanda.
Hii inaonesha kuwa Serikali ya Mama Samia haina muda wa kusikiliza majungu ya mitaani, bali imejikita katika kutengeneza soko la ndani la watu milioni 64 na soko la kikanda (EAC na SADC) lenye watu zaidi ya milioni 500.
Kwa nguvu kazi yenye ujuzi na sera rafiki zilizowekwa na Rais Samia, Tanzania sasa ni lulu ya uwekezaji. Wale wanaopiga kelele waendelee kupiga, lakini ukweli unabaki kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inajenga misingi ya chuma kwa ajili ya maisha ya baadae ya Watanzania, ikitekeleza kwa vitendo azma ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha juu ifikapo 2050.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464