
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, ametoa mwito mzito kwa Wakristo na Watanzania wote kwa ujumla kuwa wapatanishi wa kweli katika jamii ili kulinda amani na mshikamano wa taifa.
Askofu Malasusa alitoa kauli hiyo Machi 22,2026 alipokuwa akihubiri katika ibada ya uwekaji wakfu na uzinduzi wa ofisi kuu ya KKKT Dayosisi ya Konde, iliyofanyika katika usharika wa Kanisa Kuu Tukuyu mkoani Mbeya.
Alisisitiza kuwa jukumu la kulipatanisha taifa ni wito wa kila mwananchi, na ni muhimu kuchagua njia ya mazungumzo na maridhiano badala ya kuchochea migogoro na uadui miongoni mwa jamii.
Katika mahubiri yake, Askofu Malasusa alisema kuwa upatanisho ni mpango wa Mungu wenye lengo la kuondoa uadui na kuleta maelewano, hivyo waumini wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kujenga jamii yenye utulivu.
Alibainisha kuwa ili kukamilisha maana ya msalaba wa kweli, ni lazima watu wapatane wao kwa wao na si na Mungu pekee, hali itakayowezesha kazi za kimaendeleo na kiroho kusonga mbele bila vikwazo.
Aidha, aliwataka waumini wa Dayosisi ya Konde na wananchi kwa ujumla kutumia nyakati ngumu kama fursa ya kutafuta suluhu ya kudumu kupitia upatanisho badala ya kuchonganisha taifa.
Ujenzi wa ofisi hiyo mpya ya ghorofa tatu, uliogharimu takribani shilingi milioni 918 hadi sasa kati ya makadirio ya shilingi bilioni 1.3, ulitajwa kama kielelezo cha mafanikio yanayotokana na mshikamano na maridhiano.
Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi, Olais Olesenga, alibainisha kuwa mradi huo ulipata msukumo mkubwa baada ya kuwepo kwa maridhiano na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kubadilishana viwanja, hatua iliyowezesha kupatikana kwa eneo kubwa zaidi la ujenzi.
Askofu Malasusa alipongeza umoja huo na kusema kuwa mshikamano huo unapaswa kuwa kioo kwa jamii nzima katika kufikia malengo makubwa ya kimaendeleo.
Kwa upande wake, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Konde, Dk. Geoffrey Mwakihaba, alieleza kuwa ujenzi wa ofisi hiyo umechukua kipindi cha mwaka mmoja na miezi minane hadi kukamilika kwake, ikiwa ni matokeo ya juhudi za pamoja za waumini na wadau mbalimbali.
Akizungumza katika ibada hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Josephine Manase, alilishukuru kanisa kwa kuendelea kuiombea nchi na viongozi wake, akisisitiza kuwa maombi na ujumbe wa amani ni nguzo muhimu katika kudumisha utulivu wa nchi.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, serikali, na taasisi, huku ujumbe mkuu ukibaki kuwa umuhimu wa upatanisho katika ujenzi wa taifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464