` KUELEKEA SIKU YA WANAWAKE NSSF YAPANDA MITI 600 KATIKA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI MWANZA

KUELEKEA SIKU YA WANAWAKE NSSF YAPANDA MITI 600 KATIKA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI MWANZA

      

#Yatoa elimu ya umuhimu wa Hifadhi ya Jamii na utunzaji wa mazingira

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umepanda miti 600 katika shule mbili za Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka Machi 8.

Zoezi hilo limefanyika Machi 4, 2026 katika Shule ya Msingi Chasubi na Nyakabonga pamoja na Shule ya Sekondari Kayenze, likiwa na lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira pamoja na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa Hifadhi ya Jamii kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Kupitia baadhi ya wafanyakazi wake wanawake, NSSF imesema kuwa hatua hiyo inalenga kujenga uelewa wa mapema kwa vijana kuhusu umuhimu wa kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha ya uzeeni na kunufaika na mifumo rasmi ya Hifadhi ya Jamii.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Meneja wa Wananchi Waliojiajiri wa NSSF, Bi. Rehema Chuma, amesema upandaji miti unaashiria dhamira ya Mfuko huo katika kuchangia ustawi wa jamii, uyuchumi pamoja na kuhifadhi mazingira.

Ameeleza kuwa wanachama wanaojiunga na kuchangia NSSF hunufaika na mafao mbalimbali kwa mujibu wa sheria, yakiwemo mafao ya matibabu, uzeeni, ulemavu na mengineyo.

Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa wa Mwanza, Bw. Emmanuel Kahensa, amesema zoezi hilo limefanikiwa kwa ushirikiano na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ambao walitoa miche bora ya miti kwa ajili ya kupandwa katika shule hizo.

Amesisitiza kuwa ushirikiano huo unaimarisha juhudi za Serikali na taasisi zake katika kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Naye, Muhifadhi kutoka TFS, Bi. Maija Mkomwa, amesema upandaji wa miti katika taasisi za elimu ni hatua muhimu katika kujenga kizazi chenye utamaduni wa kutunza mazingira.

Walimu wakuu wa shule hizo wameishukuru NSSF kwa kushirikiana nao katika zoezi hilo, wakisema litawasaidia wanafunzi kujenga tabia ya kupenda na kulinda mazingira. Wanafunzi kwa upande wao wameahidi kuitunza miti hiyo ili iweze kuleta manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa mujibu wa NSSF, mpango huo ni sehemu ya mikakati yake ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), sambamba na kuendeleza kauli mbiu yake ya kuwajengea wanachama maisha bora ya sasa na baadaye.









Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464